Makala: Karakana ya Luban ya China yaingiza nguvu mpya kwa wahandisi vijana wa Tanzania

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 24, 2023
Makala: Karakana ya Luban ya China yaingiza nguvu mpya kwa wahandisi vijana wa Tanzania
Wanafunzi wakijifunza ufundi stadi kwenye Karakana ya Luban jijini Dar es Salaam, Tanzania, Machi 20, 2023. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)

DAR ES SALAAM - Nchini Tanzania, karakana iliyopewa jina la fundi wa China katika zama za kale Lu Ban inatoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wa eneo hilo ambao wamejaa msisimko wanapofanya kazi kwenye karakana ya magari wakiwa wamevalia ovaroli za bluu.

Ikifanya kazi chini ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) nchini Tanzania, karakana ya Luban chini ya mfumo wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) tayari imevutia wanafunzi 39, wengi wao wakiwa wanaosoma uhandisi wa magari na masomo ya teknolojia ya injini za treni.

Odhiambo Joseph Awino mwenye umri wa miaka 21, mmoja wa wanufaika wa mradi wa mafunzo ya Karakana ya Luban, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano ya hivi karibuni kwamba karakana ya Luban imemfunulia ujuzi mwingi kutoka China.

"Ujuzi na maarifa ninayopata kutoka kwenye karakana ya Luban yatanipa fursa zaidi na uzoefu katika sekta ya magari," amesema Awino, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo cha NIT anayesomea uhandisi wa magari na teknolojia ya injini za treni.

Amesema mradi wa mafunzo ya Karakana ya Luban haumfunulii tu ujuzi wa magari bali pia utamaduni wa Wachina, kwani amekuwa akijifunza lugha ya Kichina ikiwa ni sehemu ya programu hiyo ya masomo.

Awino ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mwandege wilayani Mkuranga katika Mkoa wa Pwani, Mashariki mwa Tanzania amesema anakaribisha miradi mingi ya aina hii barani Afrika, kwa kuwa Dunia imepiga hatua katika teknolojia, Afrika haipaswi kuachwa nyuma.

"Tukipata ujuzi wa kutosha miaka 10 au 20 ijayo tusitegemee sana msaada kutoka nje,” amesema mwanafunzi huyo kijana ambaye pia ana matumaini kuwa mafunzo hayo yanaweza kuendelezwa katika fani nyingine mbali na uhandisi wa magari.

"Nawashukuru washirika wetu wa China. Imekuwa heshima, na ninajisikia mwenye bahati sana kuwa sehemu ya mradi huu wa mafunzo ya karakana ya Luban. Naishukuru China kwa kutokuwa na ubinafsi na kuleta mradi huu wa mafunzo nchini Tanzania." Amesema.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha