China na Honduras zaanzisha uhusiano wa kidiplomasia (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 27, 2023
China na Honduras zaanzisha uhusiano wa kidiplomasia
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang na Waziri wa Mambo ya Nje wa Honduras Eduardo Reina wakipeana pongezi kwa kushikana mikono baada ya kutia saini taarifa ya pamoja ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili hapa Beijing, Machi 26, 2023. (Xinhua/Zhang Ling)

BEIJING - China na Honduras zimetia saini taarifa ya pamoja mjini Beijing siku ya Jumapili kuhusu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Taarifa hiyo imesema, Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Honduras, kwa kufuata maslahi na matakwa ya mataifa hayo mawili, zimeamua kutambuana na kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia katika ngazi ya balozi, kuanzia tarehe ya kutiwa saini kwa taarifa husika.

Kwa maana hiyo Honduras imekuwa nchi ya 182 kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na China.

Kuendana na mwenendo wa jumla

Taarifa hiyo iliyotiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang na Waziri wa Mambo ya Nje wa Honduras Eduardo Reina baada ya kufanya mazungumzo, inasema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Honduras inatambua kuwa kuna China moja tu duniani, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ndiyo serikali pekee halali inayowakilisha China nzima, na Taiwan ni sehemu isiyoweza kutengwa ya ardhi ya China.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Honduras itavunja "uhusiano wa kidiplomasia" na Taiwan kuanzia siku hiyo ya Jumapili na kuahidi kwamba haitaanzisha tena uhusiano au mabadilishano yoyote rasmi na Taiwan.

Kwenye mazungumzo baina yake na Qin, Reina amesisitiza kuwa Honduras inaahidi kutii kanuni ya kuwepo kwa China moja, imemuondoa "balozi" wake kutoka Taiwan, na itatangaza kufuta mikataba yote "rasmi" na Taiwan haraka iwezekanavyo.

"Honduras imefanya uamuzi muhimu wa kutambua kanuni ya kuwepo kwa China moja na kujiunga na mfumo mkuu wa Dunia, ambao unaendana kikamilifu na maslahi ya kimsingi na ya muda mrefu ya Honduras na watu wake, na pia ni chaguo la kusimama kwenye upande sahihi wa historia na upande wa nchi nyingi duniani” Qin amesema.

Ukurasa mpya wa uhusiano wa pande mbili

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali hizo mbili zimekubaliana kuendeleza uhusiano wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili kwenye msingi wa kufuata kanuni za kuheshimiana juu ya mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi, kutotumiana mabavu, kutoingiliana mambo ya ndani ya nchi, kuwa na usawa na kunufaishana na kuishi pamoja kwa amani.

Qin ametoa wito kwa pande hizo mbili kuimarisha maelewano na uratibu wao, na kuharakisha mashauriano kuhusu mikataba muhimu ya nchi mbili na taratibu za ushirikiano. Pia ameikaribisha Honduras katika kuunga mkono na kujiunga na Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, Pendekezo la Usalama wa Dunia na Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha