Bunge la Hungary laidhinisha Finland kujiunga na NATO

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 28, 2023
Bunge la Hungary laidhinisha Finland kujiunga na NATO
Wabunge wa Bunge la Hungary wakipiga kura juu ya Finland kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) mjini Budapest, Hungary, Machi 27, 2023. Bunge la Hungary Jumatatu limeidhinisha sheria inayoruhusu Finland kujiunga na Jumuiya ya NATO. (Picha na Attila Volgyi/Xinhua)

BUDAPEST - Bunge la Hungary Jumatatu limeidhinisha sheria inayoruhusu Finland kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO).

Wabunge 182 wamepiga kura ya kuunga mkono na sita kupinga, huku wabunge 11 hawakuwepo. Ukiacha chama cha mrengo wa kulia cha Mi Hazank (Nchi Yetu), vyama vyote vilipiga kura kuunga mkono Finland kujiunga na jumuiya ya NATO.

Elod Novak, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mi Hazank, alisema Ijumaa iliyopita kwamba chama chake kitapinga Finland kujiunga na NATO kwa sababu "kupanua jumuiya ya kijeshi kwenye mpaka wa Russia kutakuwa uchochezi, wakati kuwa na eneo lisiloegemea upande wowote ni maslahi ya kimataifa."

Awali Bunge la Hungary liliwasilisha muswada wa kupigia kura kuidhinishwa kwa Finland na Sweden kujiunga na NATO katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita ya Mwaka 2022, lakini tangu wakati huo bunge hilo liliamua kuendesha upigaji kura wa aina mbili kwa kila nchi.

Kabla ya upigaji kura huo wa siku ya Jumatatu, Bunge la Hungary lilituma wajumbe katika "ziara ya ukarimu" nchini Finland na Sweden, kuuliza ni kwa nini Helsinki na Stockholm zilikosoa vyombo vya kidemokrasia vya Hungary.

Finland na Sweden ziliacha sera zao za miongo kadhaa za kutohusiana au kujiunga na upande wowote wa kijeshi na kuomba kujiunga na NATO Mwezi Mei mwaka uliopita. Kabla ya kura hiyo ya Jumatatu Hungary na Uturuki ni nchi za mwisho ambazo zilikuwa zinazuia Sweden na Finland kujiunga NATO kati ya nchi wanachama 30 wa NATO ambazo tayari zimeshaidhinisha.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha