Shirika linaloongozwa na vijana nchini Zambia  lajitokeza katika kusaidia wazee wanaoishi katika mazingira magumu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 12, 2023
Shirika linaloongozwa na vijana nchini Zambia  lajitokeza katika kusaidia wazee wanaoishi katika mazingira magumu
Picha iliyopigwa Tarehe 6 Aprili 2023 ikionyesha washirika wa Shirika la Youth Changing The Mindset wakimtembelea mwanamke mzee mnufaika wa mpango huko Ndola, Mkoa wa Copperbelt, Zambia. (Picha na Lillian Banda/Xinhua)

NDOLA, Zambia, - Kuna mashirika kadhaa yanayoongozwa na vijana nchini Zambia yanayofanya kazi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana nchini humo. Hata hivyo, siyo kila siku ambapo mtu hukutana na shirika linaloongozwa na vijana ambalo huendesha programu inayotoa usaidizi wa moja kwa moja kwa wazee wenye mahitaji maalum pamoja na hatua za uingiliaji kati zinazofanywa na vijana.

Ni kwa sababu hii kwamba Shirika la Youth Changing The Mindsets (YCMO), shirika lisilo la faida ambalo linafanya kazi Ndola, Mji Mkuu wa Jimbo la Copperbelt nchini Zambia, limekuwa likijipatia sifa nyingi.

Shirika hili hutoa chakula na mavazi na katika hali mahsusi hutoa malazi kwa wazee maskini na wanaoishi katika mazingira magumu huko Chipulukusu, eneo kubwa la makazi ya watu wa kipato cha chini lililoko Mashariki mwa Ndola.

Vijana hao kutoka YCMO pia wamekuwa wakifanya ukarabati wa nyumba za wazee ili kuzifanya ziwe zenye hali nzuri zaidi kwa makazi ya wazee.

Tangu kuanzishwa kwake Juni 2022, YCMO imefikia zaidi ya wazee 50 walio katika mazingira magumu katika eneo lililotajwa hapo juu na kutoa msaada wa nyenzo na wa kisaikolojia.

"Vitu vingi vinavyotolewa kwa wazee vinatoka kwa watu wema ambao ni pamoja na vijana kutoka Chipulukusu, wafanyabiashara wenyeji na watu binafsi," amesema Comfort Mwansa, Mkurugenzi Mtendaji wa YCMO.

"Lengo letu ni kutoa huduma ya chakula kwa kila mwezi kwa angalau wazee 50. Hawa ni wazee ambao hawako katika ajira yoyote ya faida na hawana uwezo wa kujikimu." amesema.

Luckson Chisenga, Naibu Meya wa Ndola, anaona kuwa kazi ya YCMO imesaidia kupunguza mateso miongoni mwa wazee katika eneo la Chipulukusu na maeneo jirani.

"Kizazi cha wazee kilitutunza na kujitolea mengi ili kufanya maisha yetu kuwa bora. Ni zamu yetu kuhakikisha kwamba wana maisha yenye heshima." amesema Chisenga.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha