

Lugha Nyingine
Pande zinazopigana nchini Yemen zahitimisha kubadilishana idadi kubwa ya wafungwa
![]() |
Wafungwa walioachiliwa huru wakishuka kutoka kwenye ndege wakati wa kubadilishana wafungwa kwenye uwanja wa ndege wa Sana'a wa Yemen, Aprili 16, 2023. (Picha na Mohammed/Xinhua) |
ADEN, Yemen - Katika hatua muhimu ya kusuluhisha mgogoro uliodumu kwa muda mrefu nchini Yemen, pande zinazopigana nchini humo zimefanikiwa kukamilisha mchakato wa kubadilishana idadi kubwa ya wafungwa siku ya Jumapili, na jumla ya wafungwa 887 wamehusika katika mchakato huo wa siku tatu mfululizo.
Yahya Kazman, mkuu wa kamati ya mazungumzo kutoka serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, amesema mchakato wa kubadilishana wafungwa wa kundi la tatu na la mwisho ulifanyika kwa mafanikio siku ya Jumapili, na kuwasili kwa pamoja ndege tatu za Shirika la Msalaba Mwekundu kwenye uwanja wa ndege wa Sana'a na uwanja wa ndege wa Tadween huko Marib, Yemen ya Kati.
Katika muda wa siku tatu zilizopita, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) na Umoja wa Mataifa zimewezesha usafirishaji wa mamia ya wafungwa kati ya mikoa ya Yemen na Saudi Arabia kupitia viwanja mbalimbali vya ndege.
Watu mashuhuri akiwemo Nasser Mansour Hadi, ambaye ni kaka yake rais wa zamani wa Yemen Abd-Rabbu Mansour Hadi na Mahmoud Al Subeihi, waziri wa zamani wa ulinzi wa nchi hiyo ni miongoni mwa walioachiliwa huru.
Kubadilishana huko kwa wafungwa kunakuja ikiwa ni sehemu ya juhudi zinazoendelea zinazolenga kujenga kuaminiana kati ya serikali ya Yemen na wanamgambo wa Houthi, ambao wamehusika katika vita vya kikatili vya nchini humo kutoka mwishoni mwa Mwaka 2014.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma