Kampuni ya China yachangia ujenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Tanzania

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 27, 2023
Kampuni ya China yachangia ujenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Tanzania
Picha ikionyesha Bandari ya Dar es Salaam, Tanzania. (People's Daily/Huang Peizhao)

Bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania ambayo magati yake saba yalikarabatiwa na kuboreshwa na Kampuni ya China Harbour Engineering Company (CHEC) na kuanza kutumika mwaka mmoja uliopita, sasa imeongeza uwezo wake wa kuhudumia mizigo kwa asilimia 26 hadi kufikia takriban tani milioni 17.65 za mizigo kwa mwaka.

Uboreshaji huo umewezesha meli kubwa zenye uwezo wa kubeba mizigo yenye uzito wa hadi tani 70,000 kutia nanga kwenye bandari hiyo, wakati bandari hiyo ilikuwa na uwezo wa kuruhusu kutia nanga meli zenye uwezo wa kubeba mizigo yenye uzito wa tani 20,000 hapo awali.

Bian Liang, mkuu wa miradi ya uhandisi wa majini ya CHEC nchini Tanzania, ameliambia gazeti la People's Daily kuwa bandari hiyo imeboresha kwa kiasi kikubwa ufanisi wake wa kiutendaji na uwezo wa kubeba mizigo tangu magati hayo yaliyoboreshwa yaanze kutumika.

"Uboreshaji huo siyo tu kwamba unakidhi mahitaji ya Tanzania ya usafirishaji wa mizigo, lakini pia unakuza biashara ya nje ya nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na nchi nyingine zisizo na bahari barani Afrika," Bian ameeleza.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alisema, upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam una umuhimu mkubwa katika kuboresha ufanisi wa pande zote wa bandari hiyo na kukuza maendeleo ya kiuchumi ya kikanda. Aliongeza kuwa, utasukuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania, na kuwezesha biashara ya nje ya nchi zisizo na bandari katika Afrika Mashariki.

Joyce, mwanamke wa Tanzania ambaye alifanya kazi CHEC kwa miaka mitano amesema, katika miaka aliyofanya kazi kwenye mradi huo na wenzake wa China, siyo tu amekuwa mtaalamu wa rasilimali watu, lakini pia amepata uelewa wa kina wa ujenzi wa bandari. Mwaka jana, Joyce aliajiriwa kuwa mfanyakazi wa kawaida na Mamlaka ya Bandari Tanzania kutokana na utendaji wake bora.

Amesema ushirikiano wa miundombinu kati ya Tanzania na China una mchango mkubwa katika kuhimiza uhusiano kati ya watu wa nchi hizo mbili, na kuongeza kuwa uzoefu wake wa kufanya kazi CHEC ni rasilimali muhimu ya kitaaluma.

Inaelezwa kuwa mradi wa awamu ya pili wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam umeanza ili kuongeza uwezo wa bandari hiyo wa kuhudumia meli na mizigo na kuwezesha zaidi maendeleo ya kiuchumi ya Afrika Mashariki. Mradi huo unajumuisha uchimbaji, uokoaji wa vipande vya meli au mizigo baharini pamoja na ununuzi na ufungaji wa vifaa vya urambazaji.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha