Kenya yazindua programu ya mafunzo ya lugha ya Kichina kwa askari wa kada mbalimbali wa vikosi vya KDF (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 28, 2023
Kenya yazindua programu ya mafunzo ya lugha ya Kichina kwa askari wa kada mbalimbali wa vikosi vya KDF
Zhou Pingjian (Kulia), Balozi wa China nchini Kenya, akitoa hotuba kwenye hafla ya uzinduzi wa programu ya kwanza ya mafunzo ya lugha ya Kichina iliyoandaliwa mahsusi kwa ajili ya KDF jijini Nairobi, Kenya, Aprili 26, 2023. (Xinhua/Han Xu)

NAIROBI-Programu ya kwanza ya mafunzo ya lugha ya Kichina iliyoandaliwa mahsusi kwa ajili ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) imezinduliwa Jumatano huko Nairobi, Kenya, kuashiria hatua muhimu katika juhudi za kuimarisha uhusiano wa kitamaduni kati ya China na Kenya.

Balozi wa China nchini Kenya Zhou Pingjian amesema kuzinduliwa kwa programu hiyo ni hatua kubwa ya kuimarisha uhusiano wa kirafiki na maelewano kati ya raia wa China na Kenya.

Zhou ameongeza kuwa kwa kukumbatia lugha ya Kichina, vikosi hivyo vya wanajeshi wa kada mbalimbali vya Kenya vitafanya kazi kama daraja la kuhimiza mabadilishano kati ya watu huku vikiingiza uhai katika ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.

Programu hiyo iliyoanzishwa mwezi Machi kupitia ushirikiano kati ya Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Nairobi na Shule ya Elimu na Lugha ya Jeshi la Ulinzi la Kenya, tayari imesajili wanajeshi 26 kutoka kada mbalimbali.

Kozi hiyo ya mwaka mzima inalenga kuboresha ustadi wa lugha ya Kichina kati ya askari wa vikosi vya kada mbalimbali vya Kenya, kuwafahamisha utamaduni wa taifa hilo la Asia na kuwaweka kwenye msingi wa juhudi za kuhimiza diplomasia ya kitamaduni.

Mbali na mafunzo hayo ya mwaka mmoja ya lugha ya Kichina kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, wanajeshi hao 26 watakuwa wakitembelea Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Nairobi kila wiki ili kujionea utamaduni wa Kichina, zikiwemo opera, kaligrafia na sanaa za Kung-Fu.

Hivi sasa, wanajeshi hao wanakamilisha mtaala wa ngazi ya kwanza wa kozi ya umahiri wa lugha ya Kichina, na hivi karibuni watajiunga na kiwango cha pili ifikapo Desemba. Wanatarajiwa kufanya Jaribio jipya la Ustadi wa Lugha ya Kichina (HSK 3) na wale watakaofaulu watastahiki masomo zaidi nchini China.

Fredrick Leuria, Msaidizi wa Mkuu wa KDF anayehusika na Operesheni, Mipango, Mafundisho na Mafunzo, amepongeza uzinduzi wa programu hiyo akiongeza kuwa itainua uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Kenya katika ngazi mpya.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha