Familia ya Umoja wa Mataifa mjini Vienna, Austria yaadhimisha Siku ya Lugha ya Kichina

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 04, 2023
Familia ya Umoja wa Mataifa mjini Vienna, Austria yaadhimisha Siku ya Lugha ya Kichina
Wanamuziki wa China wakitumbuiza kwenye hafla ya ufunguzi wa shughuli ya Siku ya Lugha ya Kichina ya Umoja wa Mataifa huko Vienna, Austria, Mei 2, 2023. (Ujumbe wa Kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa huko Vienna/ Xinhua)

VIENNA - Familia ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini Vienna, Austria imeadhimisha Siku ya Lugha ya Kichina kwa kufanya shughuli mfululizo za kitamaduni.

Zaidi ya watu 600, wakiwemo wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yenye makao yake Vienna, wanadiplomasia na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wamehudhuria hafla kubwa ya ufunguzi wa shughuli hiyo siku ya Jumanne katika Kituo cha Kimataifa cha Vienna (VIC).

Shughuli hiyo ya mwaka huu, yenye kaulimbiu isemayo "Nyumba ya Confucius, Kitovu cha 'Ukanda Mmoja, Njia Moja'", imehusisha maonyesho mengi kuhusu Mkoa wa Shandong, Mashariki mwa China, mahali alipozaliwa mwanafalsafa wa kale wa China Confucius. Maonyesho hayo yameonyesha picha zenye alama maarufu za mkoa huo, bidhaa maalum ambazo ni alama za mkoa huo pamoja na kazi za kaligrafia za Lugha ya Kichina na picha zilizochorwa na wasanii wenyeji wa mkoa huo.

Wanamuziki kutoka Shandong pia wametumbuiza miziki ya asili ya mkoa huo kwa kutumia ala za muziki za kijadi za Kichina kwenye hafla ya ufunguzi, na kushangiliwa na watazamaji.

Katika hafla hiyo, Li Song, Mwakilishi wa Kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa mjini Vienna, amesema kuwa ikiwa ni mojawapo ya lugha sita rasmi za Umoja wa Mataifa, lugha ya Kichina imesaidia kufikisha sauti za Umoja wa Mataifa kwa Dunia na kuchangia ufanisi katika utendaji wa Umoja wa Mataifa.

Mjumbe huyo wa China ametoa wito wa kudumisha uanuai wa ushirikiano wa pande nyingi na wa kitamaduni na kuhimiza mabadilishano na ushirikiano kati ya watu.

Shughuli ya mwaka huu ya Siku ya Lugha ya Kichina katika Umoja wa Mataifa huko Vienna, ambayo itaendelea hadi Mei 5, inaandaliwa kwa pamoja na Ujumbe wa Kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa huko Vienna na Serikali ya Mkoa wa Shandong.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha