Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa asema mataifa yaliyoendelea yanapaswa kutoa haki ya mabadiliko ya tabianchi barani Afrika (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 05, 2023
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa asema mataifa yaliyoendelea yanapaswa kutoa haki ya mabadiliko ya tabianchi barani Afrika
Wanawake waliobeba maji wakielekea kwenye kambi ya Baidoa nchini Somalia, Januari 21, 2023. (Picha na Abdi/Xinhua)

NAIROBI - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hapa Jumatano kuwa nchi zilizoendelea, ambazo zinachangia kwa sehemu kubwa katika utoaji wa gesi zinazoongeza joto la sayari kama vile methane na kaboni, zinapaswa kuheshimu ahadi zao za kifedha za kusaidia Afrika kukabiliana na kuweza kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi zinazojitokeza.

Guterres, ambaye yuko katika ziara rasmi nchini Kenya, kwenye mkutano na vyombo vya habari katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi amesema kwamba nchi za eneo la kaskazini zenye maendeleo ya viwanda zina wajibu wa kimaadili kusaidia nchi za Afrika kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

"Nchi zilizoendelea lazima zifikie dola za Kimarekani bilioni 100 kwa mwaka zilizoahidiwa kwa nchi zinazoendelea na mfuko wa hasara na uharibifu uliokubaliwa huko Sharm el-Sheikh (mji wa mapumziko wa Bahari Nyekundu nchini Misri)," Guterres amesema, huku akiongeza kuwa kutoa haki ya tabianchi barani Afrika ni muhimu kwa amani, ukuaji wa uchumi na utulivu duniani.

Huku akisisitiza kwamba mpito wa kijani na uhimilivu wa siku zijazo ni dharura barani Afrika, Guterres ametoa wito kwa mataifa yaliyoendelea na yenye maendeleo ya viwanda kuunga mkono azma ya bara hilo ya kuondoa kaboni katika sekta muhimu za kiuchumi kama vile nishati.

Huku akipongeza kujitolea kwa Rais wa Kenya William Ruto kwa mpito wa asilimia 100 kuelekea nishati safi ifikapo Mwaka 2030, Guterres amesema asilimia 50 ya ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi barani Afrika inapaswa kuelekezwa kwenye miradi ya uhimilivu ili kuwezesha jamii kuhimili majanga yanayohusiana na tabianchi kama vile njaa na uhaba wa maji.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha