Mahojiano na Mkuu wa Bustani ya Wanyama ya Australia: Maisha ya panda kwenye upande wa kusini wa dunia yanaendeleaje?

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 08, 2023
Mahojiano na Mkuu wa Bustani ya Wanyama ya Australia: Maisha ya panda kwenye upande wa kusini wa dunia yanaendeleaje?
Panda Funi anayeishi Australia akila keki maalum ya panda kwenye Bustani ya Wanyama ya Adelaide wakati wa Sikukuu ya Pasaka ya mwaka 2023. Picha imetolewa na Bustani ya Wanyama ya Adelaide.

Wang Wang na Funi ni panda wawili wa kwanza kuishi kwenye upande wa kusini wa dunia. Panda hao wawili waliondoka China kwenda kwenye bustani ya wanyama ya Adelaide ya Australia mwaka 2009, na hadi sasa wamekuwa wakiishi katika nchi hiyo kwa karibu miaka 14.

Hivi karibuni, waandishi wa habari wa tovuti ya gazeti la umma wamefanya mahojiano na mkuu wa bustani hiyo Phil Ainsley, ili kufahamu hali halisi ya maisha ya hivi sasa ya panda hao wawili.

Ili kuwafanya panda hao wazoee vizuri zaidi mazingira ya Australia, mnamo mwaka 2008 bustani hiyo ya Adelaide ilijenga nyumba safi kwa ajili yao, ikiwa ni pamoja na shamba la mianzi ambalo linaweza kukidhi mahitaji yao ya malisho.

Uingizaji mianzi kutoka nchi nyingine unapigwa marufuku katika Australia, kwa hivyo panda hao wawili hawawezi kulishwa na mianzi ya kuagizwa kutoka China kama ilivyo kwa panda kwenye nchi nyingine. Lakini Ainsley anasema, Idara ya Mambo ya Maji ya Jimbo la Australia Kusini imetoa ardhi yenye eneo la ukubwa wa karibu hekta 15 ili kuwawezesha kupanda mianzi.

“Tunatoa uwanja bora wa nje ya nyumba kwa panda kucheza” ameongeza Ainsley. Wakati wa kipindi cha kuwasaidia panda hao kuzaliana, mfugaji panda hata alipanga mazoezi maalum kwa ajili ya panda dume Wang Wang, ili kumsaidia kujenga misuli yake.

Ili kuhakikisha usalama wa panda hao, bustani hiyo imeunda kikosi maalumu cha wafugaji mahsusi kwa ajili ya kuhudumia panda tu.

Ainsley amesema, “kila mwaka tunatuma ripoti kwa timu ya China, kwamba panda hao wawili wako katika afya njema sana.”

Hata hivyo, kwa sababu ya tofauti ya hali ya hewa kati ya upande wa kaskazini na kusini wa dunia, na msimu mfupi wa kutunga mimba wa panda, kuzaliana kwa panda hao wawili bado kunakabiliwa na changamoto. Majaribio yote ya siku za nyuma yaliyofanywa na bustani ya Adelaide yameshindwa.

Hivi sasa bado hakuna uhakika kama Bustani ya Adelaide itajaribu tena kumfanya panda Funi apate ujauzito tena. Inatarajiwa mwezi Mei au Juni mwaka huu, bustani ya Adelaide itafanya mashauriano na taasisi kama vile Kituo cha Utafiti wa Kuzaliana kwa Panda cha China Chengdu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha