Mashindano ya "Daraja la Lugha ya Kichina" kwa wanafunzi wa vyuo vikuu yakamilika Kaskazini mwa Misri

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 09, 2023
Mashindano ya
Mshiriki akitoa hotuba kuu wakati wa mashindano ya "Daraja la Lugha ya Kichina" kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Misri huko Ismailia, Misri, Mei 8, 2023. (Xinhua/Sui Xiankai)

ISMAILIA, Misri - Mashindano ya 22 ya "Daraja la Lugha ya Kichina" kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Misri yamehitimishwa Jumatatu katika Chuo Kikuu cha Suez Canal katika Jimbo Ismailia, Kaskazini mwa Misri.

Yakiwa yameandaliwa na Ubalozi wa China nchini Misri na Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Suez Canal, mashindao hayo yaligawanywa katika sehemu tatu, ambazo ni hotuba kuu, maonyesho ya vipaji na chemsha bongo.

Kwa maonyesho yao bora, washiriki watatu kati ya 12 waliofika fainali kutoka vyuo vikuu sita walishinda tuzo kuu.

Loay Adel Mohamed, mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Cairo na mmoja wa washindi wa tuzo kuu, alishiriki uzoefu wake mwenyewe wa kujifunza Lugha ya Kichina na kufanya onyesho la Opera ya Sichuan ya kubadilisha uso, au "bian lian," na kupigiwa makofi na shangwe nyingi za pongezi kutoka kwa watazamaji.

"Ni heshima kubwa kushinda tuzo kuu ya mashindano haya ya leo, kwa sababu sasa nina nafasi ya kushindana nchini China na kuonyesha upendo wangu kwa utamaduni wa China," ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

Balozi wa China nchini Misri Liao Liqiang amesema kuwa hivi sasa watu wa China na Misri wanafanya kazi kwa bidii ili kutimiza ndoto zao kuu.

"Ninatumai kuwa wanafunzi wa Misri wataweza kuielewa China kwa undani zaidi kwa kujifunza Lugha ya Kichina, ili kutoa mchango katika maendeleo ya pamoja ya nchi zote mbili," Liao amesema.

Nasser Mandour, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Suez Canal amesema, kutokana na maendeleo ya haraka ya uchumi na teknolojia ya China katika miaka ya hivi karibuni, wanafunzi wengi zaidi kutoka duniani kote wanataka kujifunza Lugha ya Kichina.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha