Maonyesho ya safari za utalii ya Afrika (Indaba ya Utalii) yafunguliwa huko Durban nchini Afrika Kusini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 10, 2023
Maonyesho ya safari za utalii ya Afrika (Indaba ya Utalii) yafunguliwa huko Durban nchini Afrika Kusini
Picha iliyopigwa Mei 3, 2017, ikionyesha mandhari ya pwani ya Durban katika Jimbo la KwaZulu-Natal, Afrika Kusini. (Xinhua/Zhai Jianlan)

DURBAN, Afrika Kusini - Indaba ya safari za utalii ya Afrika ambayo ni shughuli maalumu ya kutangaza na kuonyesha utalii wa Afrika imeanza Jumatatu katika Mji wa Durban, KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini, huku Waziri wa Utalii wa nchi hiyo Patricia de Lille akitoa wito wa ushirikiano kati ya nchi za Afrika ili kukuza sekta ya utalii.

De Lille amesema shughuli hiyo ya utalii inatoa fursa ya mawasiliano ya ana kwa ana, kujenga mitandao ya kibiashara, kubadilishana mawazo, na kuunda ushirikiano ambao utaimarisha kufufuka kwa sekta hiyo.

Zaidi ya nchi 20 za Afrika zinashiriki katika shughuli hiyo, ambayo itakamilika Alhamisi, ambapo zaidi ya bidhaa 350 za utalii zitaonyeshwa.

"Tumedhamiria kufufua sekta ya utalii na kuhakikisha tunaendelea kuchangia katika kutengeneza ajira na kukuza uchumi wa bara hili. Ni muhimu tushirikiane kuitangaza Afrika kama kivutio cha utalii kinachopendelewa kwa utalii wa mapumziko na shughuli za kibiashara. Sekta za umma na za kibinafsi lazima ziungane ili kuonyesha bidhaa mbalimbali za Afrika Bara na kuimarisha teknolojia, kuchochea uvumbuzi, na kuunda uzoefu wa kukumbukwa kwa wageni," amesema De Lille.

Indaba ya Safari za utalii za Afrika ni maonyesho ya biashara ya utalii wa mapumziko ya Afrika, yanayomilikiwa na Idara ya Utalii ya Afrika Kusini, ikiwa na madhumuni mahususi ya kuunda ufikiaji wa soko kwa idadi kubwa ya bidhaa za utalii wa mapumziko za Afrika.

Maonyesho hayo ya biashara ya utalii yalitanguliwa na Siku maalum ya Kujenga Mitandao ya Fursa za Biashara (BONDay) ambayo inalenga kuunda jukwaa la mawazo ya uongozi, kubadilishana maarifa na kupata mambo mapya zaidi katika mitindo na maarifa ya kimataifa na barani Afrika. Programu ya BONDay imetengenezwa kwa ushirikiano wa karibu na mashirika ya utalii duniani, wataalamu wa bara hilo na mashirikisho ya tasnia ya utalii.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha