Hafla ya kutoa stempu za kumbukumbu za miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Hispania yafanyika Hengshui, China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 11, 2023
Hafla ya kutoa stempu za kumbukumbu za miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Hispania yafanyika Hengshui, China
Picha hii ikionesha Stempu za kumbukumbu za “Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya China na Hispania”.

Tarehe 10, Mei, hafla ya kutoa kwa mara ya kwanza stempu za kumbukumbu za “maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Hispania” ilifanyika huko Hengshui, Mkoa wa Hebei wa China.

Ili kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Hispania, Shirika la Posta la China pamoja na upande wa Hispania tarehe 10, Mei zimetoa seti ya stempu mbili za kumbukumbu ya “Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhusiano wa Kidiplomasia wa China na Hispania”.

Picha kwenye stempu hizi zinahusu Ziwa Hengshui la China na Ziwa Fuente Piedra la Hispania, zikionesha mandhari nzuri na sifa za mazingira asilia ya maziwa hayo mawili.

Mwongozaji wa hafla hiyo, ambaye pia ni mtaalamu kutoka Hispania wa tovuti ya Gazeti la Umma (People’s Daily Online), Alvaro Lago, alisema kwenye hafla hiyo kwamba, mamia ya maelfu ya ndege huja kwenye Ziwa Hengshui kwa ajili ya kuzaliana kila wakati wa majira ya mchipuko, jambo ambalo limemfanya akumbuke hali kama hiyo katika mji wa nyumbani kwao wa Malaga. Amesema Ziwa Hengshui na Ziwa Fuente Piedra yote yana thamani kubwa, kama ilivyo kwa urafiki kati ya nchi hizo mbili.

Zaidi ya miaka 2000 iliyopita, njia ya hariri ya kale ya ardhini iliunganisha mji mkuu wa kale wa China Chang’an pamoja na jiji Tarragona la Hispania. Jamhuri ya Watu wa China na Ufalme wa Hispania zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia tarehe 9, Machi, 1973. Mnamo mwezi Novemba, 2005, nchi hizo mbili zilianzisha uhusiano wa kiwenzi wa kimkakati wa pande zote.

Inafahamika kuwa, stempu hizi za kumbukumbu zimebuniwa na Ma Lihang na kuchapishwa na kampuni ya Kiwanda cha Stempu cha Beijing, huku kukiwa na mipango ya kuchapisha jumla ya seti milioni 6.9. Stempu hizi zitauzwa kwenye matawi ya posta yaliyoodheshwa nchini China na pia kwenye maduka ya mtandaoni ya Posta ya China, na zitauzwa kwa miezi sita.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha