Waziri wa Utalii wa Afrika Kusini asema nchi za BRICS zina uwezo wa kuongeza wasafiri wa utalii kwenda Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 11, 2023
Waziri wa Utalii wa Afrika Kusini asema nchi za BRICS zina uwezo wa kuongeza wasafiri wa utalii kwenda Afrika
Picha ya angani, iliyopigwa Juni 17, 2022, ikionyesha jengo la makao makuu ya Benki ya Maendeleo Mapya(NDB), inayojulikana pia kama Benki ya BRICS, huko Shanghai, Mashariki mwa China. (Xinhua/Fang Zhe)

JOHANNESBURG - Afrika Kusini na nchi nyingine za Afrika zinatarajia ongezeko la watalii kutoka nchi za BRICS kufuatia kuondolewa kwa vikwazo vilivyowekwa kukabiliana na UVIKO-19, kwa mujibu wa Waziri wa Utalii wa Afrika Kusini Patricia De Lille.

De Lille ameyasema hayo kwenye Mazungumzo ya Afrika kuhusu Utalii, ambayo ni shughuli ya pembezoni mwa Indaba ya Safari za Utalii ya Afrika, maonyesho ya kibiashara ya utalii yaliyoanza Jumatatu, akiwahutubia mawaziri wa Afrika na viongozi wengine wa utalii katika hoteli moja mjini Durban, KwaZulu-Natal, Jumatatu usiku.

"Na ingawa watalii hawa wanatoka katika masoko yaliyozoeleka kama vile Uingereza, Ulaya na Marekani, masoko muhimu kama vile kurejea kwa safari kutoka China ni jambo muhimu sana. Nchi kama China, India na Brazil zina watu wa tabaka la kati wanaoibukia tayari kutalii Afŕika Kusini na Bara la Afrika. Kukuza utalii ni mojawapo ya maeneo ambayo BRICS inayangazia," amesema De Lille. BRICS ni kifupi cha ushirikiano wa nchi zenye masoko yanayoibukia unaojumuisha Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.

Ameeleza kuwa Brazil ilionyesha ongezeko la juu zaidi la watalii wanaoingia Afrika Kusini kwa miezi mitatu ya kwanza ya 2023, ikiwa ni zaidi kuliko nchi nyingine yoyote ya Amerika ya Kati na Kusini. De Lille amekaribisha kurejeshwa kwa safari za ndege za moja kwa moja za shirika la ndege la Brazil LATAM kati ya Johannesburg na Sao Paulo. Amesema kuwa BRICS inakua na ina uwezo wa kuongeza biashara na nchi za Afrika.

De Lille amewaambia mawaziri na wajumbe wa Afrika kwamba Afrika Kusini itakuwa mwenyeji wa mkutano wa BRICS Mwezi Agosti. Amesema ushiriki wa Afrika Kusini katika BRICS utaendeleza Afrika na kujenga Dunia bora.

Afrika Kusini ilichukua nafasi ya mwenyekiti wa BRICS mnamo Januari 1, 2023, ikichukua usukani kutoka China.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha