Uchaguzi wa Rais wa Uturuki huenda ukaenda kwenye duru ya marudio baada ya asilimia 93 ya kura zote kuhesabiwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 15, 2023
Uchaguzi wa Rais wa Uturuki huenda ukaenda kwenye duru ya marudio baada ya asilimia 93 ya kura zote kuhesabiwa
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (wa kwanza kushoto) akipiga kura kwenye kituo cha kupigia kura mjini Istanbul, Uturuki, Mei 14, 2023. Raia wa Uturuki walielekea kwenye uchaguzi siku ya Jumapili kwa ajili ya uchaguzi wa aina mbili yaani wa rais na wabunge ambao unaweza kuleta mwelekeo mpya wa kisiasa wa Uturuki kwa miaka ijayo. Wapiga kura wapatao milioni 61 wamesajiliwa kupiga kura zao. Takriban wapiga kura milioni 3.5 wanaoishi nje ya nchi wameitwa kupiga kura zao mapema. Zaidi ya Waturuki milioni 1.76 wanaoishi nje ya nchi wamepiga kura zao katika balozi za kidiplomasia na milango ya forodha kati ya Aprili 27 na Mei 9. (Mustafa Kaya/Kitini kupitia Xinhua)

ANKARA – Uturuki ilikuwa na kila dalili za kuelekea kwenye uchaguzi wa marudio wa urais wakati hesabu ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi mkuu wa Jumapili ilionyesha hakuna mgombea aliyepata kura juu ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa ili kuwezesha kushinda moja kwa moja, kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotolewa na Mamlaka za Uchaguzi za Uturuki na kutangazwa na Shirika la Habari la Uturuki, Anadolu mapema Jumatatu.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Anadolu yanaonyesha Rais aliyeko madarakani sasa wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anaongoza kwa kura zaidi ikilinganishwa na mpinzani wake mkuu Kemal Kilicdaroglu, lakini pengo lilipunguzwa kadri kura nyingi zilivyokuwa zikihesabiwa.

Erdogan alikuwa amepata asilimia 49.67 ya kura wakati asilimia 93 ya kura zote zilipokuwa tayari zimehesabiwa, dhidi ya asilimia 44.59 ya kura za kiongozi wa upinzani Kemal Kilicdaroglu, shirika hilo la Anadolu limeripoti. Mgombea wa tatu Sinan Ogan alipata asilimia 5.3 ya uungwaji mkono.

Iwapo hakuna mgombeaji urais atakayepata kura nyingi za kutosha, yaani zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa katika duru ya kwanza, uchaguzi wa marudio utaratibiwa kati ya wagombea wawili waliopata kura nyingi zaidi Tarehe 28 Mei.

Wakati masanduku ya kura katika uchaguzi wa wabunge nayo yakimalizika kuhesabiwa, matokeo yasiyo rasmi yanaonyesha kuwa Muungano wa People's Alliance unaoundwa na chama tawala cha Rais Erdogan cha Justice and Development Party (AKP), Chama cha Nationalist Movement (MHP), Chama cha New Welfare na Chama cha Great Union ulikuwa na wabunge 323, ikiwa ni idadi ya juu zaidi kati ya miungano mitatu ambayo inawania nafasi za bunge lenye wajumbe 600.

Wapiga kura takribani milioni 61 wamesajiliwa kupiga kura zao. Takriban wapiga kura milioni 3.5 wanaoishi nje ya nchi wameitwa kupiga kura zao mapema. Idadi ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki ilikuwa juu kwa karibu asilimia 80. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha