Mradi wa kufua umeme kwa maji wa CPEC wakamilisha hatua ya ujenzi wa kingo za juu za bwawa nchini Pakistan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 16, 2023
Mradi wa kufua umeme kwa maji wa CPEC wakamilisha hatua ya ujenzi wa kingo za juu za bwawa nchini Pakistan
Picha iliyopigwa Mei 15, 2023 ikionyesha bwawa la mradi wa kuzalisha umeme kwa nishati ya maji wa Suki Kinari chini ya Ukanda wa Kiuchumi wa China-Pakistani (CPEC) katika Wilaya ya Mansehra, Jimbo la Khyber Pakhtunkhwa, Pakistan. (CGGC/Xinhua)

ISLAMABAD - Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa nishati ya Maji wa Suki Kinari wa Pakistan katika sehemu ya kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo umekamilisha hatua ya ujenzi wa kingo za juu za bwawa siku ya Jumatatu, na kuashiria kuingia katika hatua mpya ya ujenzi.

Kuwekwa kwa kingo za juu za bwawa la zege kwenye Mto Kunhar kwa mafanikio kutasaidia kuendeleza ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme chini ya Ukanda wa Kiuchumi wa China na Pakistan (CPEC), ulioko katika wilaya ya Mansehra katika Jimbo la Khyber Pakhtunkhwa katika nchi hiyo ya Asia Kusini.

Akielezea hatua ya kumalizika kwa ujenzi wa kingo hizo za mradi huo wa kuzalisha umeme wenye nguvu za megawati 884 kuwa mafanikio makubwa, Chen Jiangbo, Naibu Meneja wa mradi wa Kundi la Kampuni ya China Gezhouba, ambayo inawekeza na kutekeleza mradi huo, amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za pamoja zilizofanywa na wajenzi wa China na Pakistani licha ya changamoto nyingi.

“Mradi huo wa kuzalisha umeme kwa maji ulianza kujengwa Januari 2017 kwa uwekezaji wenye thamani ya jumla ya dola za Kimarekani bilioni 1.96. Unatarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa muundo wa nishati wa Pakistan, na kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo,” amesema Chen.

Ameongeza kusema kuwa, mara mradi huo utakapoanza kufanya kazi, kila mwaka utazalisha kilowati bilioni 3.21 za umeme safi kwa saa, kuchukua nafasi ya tani milioni 1.28 za makaa ya mawe na kupunguza tani milioni 2.52 za utoaji hewa ya kaboni kwa mwaka.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha