China yatandaza zulia jekundu kuwakaribisha viongozi wa Nchi za Asia ya Kati

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 18, 2023
China yatandaza zulia jekundu kuwakaribisha viongozi wa Nchi za Asia ya Kati
Rais wa Kazakh Kassym-Jomart Tokayev akiwasili Xi'an, Mkoa wa Shaanxi, Kaskazini-Magharibi mwa China, Mei 17, 2023. (Xinhua/Li Yibo)

XI'AN – China siku ya Jumatano iliandaa hafla ya kuwakaribisha kwa furaha viongozi wa Nchi za Asia ya Kati ambao wanawasili kwa kuhudhuria mkutano muhimu wa viongozi wakuu unaotarajiwa kuweka mwelekeo mpya wa ushirikiano kati ya China na Nchi za Asia ya Kati.

Maandalizi na kila kitu kiko tayari katika mji wa Kaskazini-Magharibi mwa China wa Xi'an, kituo cha kihistoria cha kuanzia kwa Njia ya Kale ya Hariri, kwa ajili ya Mkutano wa Viongozi Wakuu wa China na Nchi za Asia ya Kati, ambao umepangwa kufanyika leo Alhamisi na Ijumaa.

Mkutano huo, ambao ni wa kwanza wa kukutana ana kwa ana kati ya viongozi wakuu wa China na nchi tano za Asia ya Kati, ambazo ni Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan, utaongozwa na Rais Xi Jinping wa China.

Rais Xi ataeleza msimamo wa China kuhusu namna ya kujenga jumuiya ya China na Nchi za Asia ya Kati yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya na kutoa mapendekezo kadhaa ya maendeleo ya muda mrefu ya ushirikiano kati ya nchi hizo sita.

Rais Xi pia atatangaza hatua mfululizo za kivitendo ili kupanga mpango kwa pande zote kuhusu mwelekeo wa ushirikiano kati ya China na Nchi za Asia ya Kati.

Kiongozi wa kwanza kuwasili Xi'an alikuwa Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev. Rais wa Tajikistan Emomali Rahmon na Rais wa Kyrgyzstan Sadyr Japarov pia waliwasili siku hiyo ya Jumatano.

Rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev na Rais wa Turkmenistan Serdar Berdimuhamedov watawasili leo siku ya Alhamisi. Karamu ya kuwakaribisha itafanyika kwa viongozi hao watano.

Viongozi hao ambao wamefika walilakiwa kwa furaha na maonyesho mbalimbali ya michezo ya sanaa yakiwemo ya ngoma za asili za Shaanxi kwenye uwanja wa ndege.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha