Zambia yaeleza nia ya kuvutia uwekezaji wa China kwenye Maonyesho ya Uchumi na Biashara kati ya China na Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 18, 2023
Zambia yaeleza nia ya kuvutia uwekezaji wa China kwenye Maonyesho ya Uchumi na Biashara kati ya China na Afrika
Picha ya kumbukumbu ikionyesha watembeleaji wa maonyesho wakipiga picha wakati wa Maonyesho ya Pili ya Uchumi na Biashara kati ya China na Afrika huko Changsha, Mji Mkuu wa Mkoa wa Hunan, China, Septemba 29, 2021. (Xinhua/Chen Sihan)

LUSAKA - Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zambia Chipoka Mulenga alisema siku ya Jumanne kuwa Zambia ina nia ya kuvutia uwekezaji zaidi wa China itakaposhiriki katika Maonyesho yajayo ya Tatu ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika.

Maonyesho hayo ya tatu, yatakayofanyika chini ya kaulimbiu isemayo "Maendeleo ya Pamoja kwa Mustakabali wa Pamoja," yataanza Juni 29 hadi Julai 2 katika Mkoa wa Hunan, Katikati mwa China. Yakiwa yalifanyika kwa mara ya kwanza Mwaka 2019, maonyesho hayo ni jukwaa kuu la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Afrika.

Mulenga amesema ataongoza ujumbe wa wafanyabiashara katika maonyesho hayo, na jumla ya kampuni 21 hadi sasa zimeonyesha nia ya kuwa sehemu ya ujumbe huo.

"Ndiyo, Zambia inatarajia kushiriki katika maonyesho hayo. Hakika, nchi yangu ina shauku ya kuhakikisha tunapanua sehemu yetu ya soko na uvutiaji wa uwekezaji kutoka sehemu mbalimbali za Dunia. Na fursa hii ambayo China imeitoa kwa Afrika na nchi nyingine nyingi ni jambo ambalo hatutaki kuachwa," amesema katika mahojiano.

Mulenga amesema kampuni nyingi za kibiashara ndogo na za kati zilionyesha nia ya kuwa sehemu ya ujumbe huo wakati wa mazungumzo na Ubalozi wa China nchini Zambia, na ni muono wa serikali kuwa kampuni za kibiashara ndogo na za kati ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

"Zambia ina nia ya kuvutia uwekezaji zaidi na kuongeza thamani ya malighafi yake," amesema, huku akiongeza kuwa kushiriki shughuli kama maonyesho hayo kutawezesha kampuni za Zambia kuanzisha uhusiano wa kibiashara na vile vile ubia wa kimkakati.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha