Kutoka milimani hadi duniani—Safari ya maendeleo ya kahawa ya Yunnan (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 19, 2023
Kutoka milimani hadi duniani—Safari ya maendeleo ya kahawa ya Yunnan
Wakulima wa kahawa wakikausha matunda ya kahawa kwenye mashamba ya kahawa ya kijiji cha Mangmao, mkoani Yunnan, Kusini Magharibi mwa China. (Picha na Mao Zunhui/Tovuti ya Gazeti la Umma)

Yunnan ni mkoa unaozalisha kahawa wenye eneo kubwa zaidi la kupanda na kuvuna kahawa nyingi zaidi nchini China. Kahawa ya Yunnan inasifiwa kuwa mojawapo ya kahawa bora zaidi duniani kwa ladha yake ya kipekee.

Katika miaka ya hivi karibuni, kahawa ya Yunnan imekuwa maarufu zaidi kwa watumiaji wa ndani na nje ya China. Starbucks, Nestle, Luckin coffee, Manner na chapa nyingine nyingi zimezindua bidhaa mbalimbali za maharagwe ya kahawa ya Yunnan. Starbucks ilianzisha kituo cha kwanza cha usaidizi kwa wakulima wa kahawa katika eneo la Asia-Pasifiki huko Pu'er, mkoani Yunnan, na kituo cha kukusanya maharagwe ya kahawa kilichoanzishwa na Manner Coffee huko Menglian, Yunnan kimekuwa sehemu ambapo wakulima wa kahawa wanakwenda mara kwa mara.

Takwimu zinaonyesha kuwa, katika nusu ya kwanza ya 2022, kiasi cha mauzo ya nje ya kahawa ya Yunnan kilifikia tani 18,000, ikiwa na thamani ya yuani milioni 550, na bidhaa hizo zimesafirishwa na kuuzwa katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU), Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini Mashariki (ASEAN), Marekani, Mashariki ya Kati na maeneo mengine.

Kutoka milimani hadi duniani, kahawa ya Yunnan inazidi kuwa chapa mpya ya uchumi wazi wa China.

Hata hivyo, hapo zamani Yunnan ilikuwa ikichukuliwa kama eneo la kijadi la uzalishaji wa chai nchini China. Kwa hivyo, ni kwa namna gani kahawa, ambayo ni bidhaa ya kigeni, imeweza kueneza harufu yake duniani kote kutokea hapa Yunnan?

Kahawa iliingia Yunnan mwishoni mwa karne ya 19, lakini maendeleo yake ya mapema yalikuwa yasiyoratibiwa vizuri. Mnamo Mwaka 1988, ili kupunguza athari za vituo vya uzalishaji wa kahawa vya Amerika Kusini kwenye bei ya kahawa, Nestle na kampuni nyingine zilianza kuunga mkono maendeleo ya tasnia ya kienyeji ya kahawa ya Yunnan. Kufikia mwisho wa 1997, uzalishaji wa kahawa katika Mkoa wa Yunnan ulikuwa umechangia 83% ya uzalishaji wa nchi nzima ya China.

Wakati chapa za kimataifa zikimiminika, kampuni za kienyeji huko Yunnan pia zinajitegemea. Mwaka 2011, Ye Ping, mwanamke wa Kabila la Wa-wa kutoka kijiji cha Mangmao, Wilaya ya Menglian, Mji wa Pu'er, mkoani Yunnan, aliwaongoza wanakijiji kuanzisha Ushirika wa Kitaalamu wa Wakulima wa Kahawa wa Tianyu Menglian. Kahawa zilizozalishwa na ushirika huo zilikabidhiwa kwa wawakilishi wa nchi 14 wanachama za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Zhang Jun, mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa mnamo Mei 2021, hivyo kuifanya kahawa ya Yunnan kuwa maarufu ndani na nje ya China.

Kwa vile watumiaji wana mahitaji ya juu zaidi ya ubora wa kahawa, wakulima wa kahawa huko Yunnan walianza kuchunguza njia ya kuzalisha kahawa zenye ubora wa juu. Mnamo Mwaka 2022, maharagwe ya kahawa yaliyopandwa na mkulima wa Yunnan Pan Qizuo yalichaguliwa katika "Orodha Chaguo ya Starbucks" kwa mara ya tatu. Katika Maonyesho ya pili ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE), Starbucks ilichagua maharagwe ya kahawa kutoka Shamba la Zuoyuan kama kahawa wakilishi ya Yunnan, ikionyesha ubora wa juu wa kahawa ya Yunnan kwa wageni wa duniani kote.

Katika miaka ya hivi karibuni, Mkoa wa Yunnan umetoa mfululizo wa nyaraka za mwongozo kwa ajili ya maendeleo ya tasnia ya kahawa. Chini ya mwongozo wa sera, kiwango cha ubora wa hali ya juu wa maharagwe ya kahawa ya Yunnan kimeinuka kwa kiasi kikubwa.

Kushamiri kwa tasnia ya kahawa pia kumevutia vijana wa Yunnan kurejea nyumbani kwao. Vijana hawa wamerejea na mbinu za usimamizi uliokomaa zaidi na mbinu za upandaji.

Kwa miaka mingi iliyopita, kahawa imekuwa na maana zaidi kwa wakulima wenyeji kuliko chanzo cha mapato na kuwa utambulisho wa kitamaduni.

Hivi sasa, Pu'er ina wakulima wengi wanaopanda chai na pia kahawa. Wakulima hawa huvuna matunda ya kahawa wakati wa majira ya baridi na kuchuma majani ya chai katika majira ya mchipuko.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha