Rais Xi Jinping asema Uhusiano wa China na Nchi za Asia ya Kati unachangia amani na utulivu wa kikanda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 20, 2023
Rais Xi Jinping asema Uhusiano wa China na Nchi za Asia ya Kati unachangia amani na utulivu wa kikanda
Rais Xi Jinping wa China, pamoja na Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev, Rais wa Kyrgyzstan Sadyr Japarov, Rais wa Tajikstan Emomali Rahmon, Rais wa Turkmenstan Serdar Berdimuhamedov na Rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev, wakikutana na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mafanikio kwa Mkutano wa Viongozi Wakuu wa China na Nchi za Asia ya Kati uliofanyika Xi 'an, Mkoa wa Shaanxi, Kaskazini Magharibi mwa China, Mei 19, 2023. (Xinhua/Li Xueren)

XI'AN - Kwa juhudi za pamoja, uhusiano kati ya China na Nchi za Asia ya Kati utaongeza nishati chanya katika kuleta amani na utulivu wa kikanda, Rais wa China Xi Jinping amesema Ijumaa alipokutana na waandishi wa habari baada ya kuhitimishwa kwa mafanikio kwa Mkutano wa Viongozi Wakuu wa China na Nchi za Asia ya Kati.

Rais Xi, pamoja na Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev, Rais wa Kyrgyzstan Sadyr Japarov, Rais wa Tajikstan Emomali Rahmon, Rais wa Turkmenstan Serdar Berdimuhamedov na Rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev, kwa pamoja walikutana na waandishi wa habari.

Nchi hizo sita kwa pamoja zimetia saini Azimio la Xi'an la Mkutano wa Viongozi Wakuu wa China na Nchi za Asia ya Kati, kupitisha orodha ya matokeo ya mkutano huo, na kuweka dira ya maendeleo ya baadaye ya uhusiano wa China na Nchi za Asia ya Kati, Rais Xi amesema.

Amebainisha kuwa kwenye azimio hilo nchi hizo sita zimeazimia kufanya kazi pamoja ili kukabiliana na changamoto na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya karibu ya China na Nchi za Asia ya Kati yenye mustakabali wa pamoja.

“China na nchi za Asia ya Kati zitaungana mkono kithabiti katika masuala yanayohusu maslahi yao ya msingi kama vile mamlaka, uhuru, usalama na ukamilifu wa ardhi,” Rais Xi amesema.

Ameongeza kuwa Nchi za Asia ya Kati zinatambua kikamilifu umuhimu wa safari ya China ya maendeleo ya kisasa kwa maendeleo ya Dunia na kusisitiza ahadi yao thabiti katika kufuata kanuni ya kuwepo kwa China moja.

Viongozi hao wakuu wa China na Nchi za Asia ya Kati katika azimio hilo la Xi’An wamekubaliana masuala mengine kadhaa kama vile, kujenga muunganisho wa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, kuhimiza mabadilishano kati ya watu kutoka pande zote, kupambana na aina zote za ugaidi, makundi ya kujitenga na yenye itikadi kali, pamoja na ulanguzi wa dawa za kulevya na uhalifu wa kupangwa wa kimataifa, kuunga mkono na utayari wa kutekeleza Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, Pendekezo la Usalama wa Dunia na Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia na wametangaza kuanzisha rasmi Utaratibu wa Mkutano wa Viongozi Wakuu wa China na Nchi za Asia ya Kati.

Pande hizo mbili -- China na nchi za Asia ya Kati -- zitabadilishana kuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaokuwa unafanyika kila baada ya miaka miwili.

Mkutano unaofuata utafanyika Kazakhstan Mwaka 2025.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha