Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa asema eneo la biashara huria la Afrika ni kichocheo cha ukuaji endelevu wa uchumi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 25, 2023
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa asema eneo la biashara huria la Afrika ni kichocheo cha ukuaji endelevu wa uchumi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Mei 17, 2023. (Xinhua/Xie E)

UMOJA WA MATAIFA - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumzia mchango muhimu wa Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) katika maendeleo endelevu ya bara hilo siku ya Jumatano.

"Tukiongozwa na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063, lazima tuongeze juhudi zetu na kutumia uwezo kamili wa biashara na maendeleo ya viwanda ili kuendeleza ukuaji endelevu na shirikishi," afisa huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika siku ya mwisho ya mikutano ya Msururu ya Majadiliano ya Afrika huko New York, ambapo mwaka huu lengo lilikuwa katika kuongeza kasi ya utekelezaji wa AfCFTA – eneo la biashara ambalo litakuwa kubwa zaidi duniani.

"Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika linawekwa kuwa injini ya ukuaji huo," amebainisha Guterres.

"Ukuaji mkubwa wa uchumi ambao nchi nyingi za Afrika zilipata kabla ya UVIKO-19 ulipotea kutokana na janga hili," Guterres amesema, huku akiangazia hitaji la kuongeza juhudi kuelekea soko moja la biashara katika bara.

Utekelezaji kamili wa AfCFTA unaweza kuzalisha mapato ya hadi asilimia 9 ifikapo Mwaka 2035, kwa mujibu wa makadirio ya hivi karibuni. Hii inaweza kuondoa watu hadi milioni 50 kutoka kwenye umaskini uliokithiri na kupunguza kukosekana kwa usawa wa mapato, ameongeza.

"Tunahitaji mageuzi ya kimsingi ya mfumo wa fedha duniani ili Afrika iwakilishwe katika ngazi ya juu," amesema.

Vikwazo vinavyorudisha nyuma uwezo wa biashara na uzalishaji wa ndani wa Afrika lazima pia vivunjwe, ikiwa ni pamoja na kuondoa ushuru, kujenga minyororo ya ugavi ya “Made in Africa,” na kuoanisha kanuni ambazo zinaweza kuwezesha uwekezaji.

Hoja yake ya tatu imeangazia miundombinu ya nishati na ya kidijitali, ambayo ni muhimu kwa nchi za Afrika katika kujenga uwezo wao wa utengenezaji bidhaa na kutumia uwezo kamili wa uvumbuzi na ujasiriamali.

Mikutano ya Msururu wa Majadiliano ya Afrika huleta pamoja watoa maamuzi, wataalam, wasomi, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, vijana na wadau wengine kutazama changamoto na fursa zinazoathiri bara hilo.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha