Ndege ya C919 ambayo ni ya kwanza kuundwa na China yaanza kufanya kazi kibiashara

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 29, 2023
Ndege ya C919 ambayo ni ya kwanza kuundwa na China yaanza kufanya kazi kibiashara
Ndege kubwa ya abiria ya C919, ambayo ni ndege kubwa ya kwanza kuundwa na China yenyewe, ikipaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Shanghai Hongqiao huko Shanghai, Mashariki mwa China, Mei 28, 2023. C919 imekamilisha safari yake ya kwanza ya kibiashara kutoka Shanghai hadi Beijing siku ya Jumapili. (Xinhua)

SHANGHAI/BEIJING - C919, ndege kubwa ya abiria ya kwanza kuundwa na China yenyewe, imekamilisha kwa mafanikio safari yake ya kwanza ya kibiashara kutoka Shanghai hadi Beijing siku ya Jumapili, kuashiria kuingia kwake rasmi katika soko la usafiri wa anga.

Ndege hiyo inayoendeshwa na Shirika la Ndege la China Eastern, ilipaa kwa nambari ya utambuzi wa safari MU9191 saa 4:32 asubuhi kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Shanghai Hongqiao ikiwa na abiria 128.

Ndege hiyo ilipokelewa kwa saluti ya maji baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing saa 2:31 Mchana.

"Uendeshaji wa kibiashara wa C919 unamaanisha kwamba kwa mara ya kwanza, soko la usafiri wa anga la China limepata ndege kubwa ya kwanza kuundwa na nchi yenyewe," amesema Wei Yingbiao, Naibu Mkuu wa Shirika la Ndege la Biashara la China (COMAC), ambalo ni muundaji wa ndege hiyo ya C919.

Safari ya Kihistoria

Shangwe na nderemo zilitawala ndani ya ndege hiyo iliyopewa utambuzi wa safari MU9191 Jumapili. Wakipeperusha bendera ndogo za taifa la China, abiria waliimba nyimbo za kusherehekea mafanikio hayo maalum kwao na kwa tasnia ya usafiri wa anga nchini China.

Abiria mmoja anayetumia jina la ubini la Li amesema ameridhishwa na safari hiyo. "Uzoefu ulikuwa mzuri. Sikusikia kelele nyingi, na sehemu ya kupita abiria ndani ya ndege na siti zina nafasi kubwa."

Ndege hiyo sasa itaanza kuendeshwa kwa mara ya kwanza kibiashara kwenye njia ya Shanghai Hongqiao-Chengdu Tianfu ya Shirika la Ndege la China Eastern. Baada ya kuundwa na kukabidhiwa ndege nyingine zaidi, Ndege ya C919 itaruka hatua kwa hatua kwenye njia zaidi, amesema Feng Dehua, Naibu Meneja Mkuu wa shirika hilo la ndege.

Matarajio makubwa

Tangu mradi wa C919 uzinduliwe Mwaka 2007, umepitia safari ndefu ya kubuni, kuunda, majaribio ya safari za ndege, na hatimaye kuuzwa kibiashara. Watu karibu 300,000 wameshiriki katika maendeleo ya uundaji wa ndege hiyo.

Novemba 2015, ndege ya kwanza ya C919 iliondoka kwenye kiwanda cha uundaji huko Shanghai. Mwaka 2017, ndege hiyo ilifanya safari ya kwanza kwa mafanikio.

Desemba 2022, Shirika la Ndege la China Eastern lilipokea ndege ya kwanza ya C919 kuwahi kuwasilishwa duniani kote.

Hadi sasa, C919 imepata oda za ndege 1,061 kutoka kwa wateja mbalimbali, imesema COMAC.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha