Daraja linalojengwa na China linalounganisha jamii muhimu katika Nchi ya Cote d'Ivoire lakaribia kukamilika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 29, 2023
Daraja linalojengwa na China linalounganisha jamii muhimu katika Nchi ya Cote d'Ivoire lakaribia kukamilika
Picha hii ya angani iliyopigwa Tarehe 25 Mei, 2023 ikionyesha magari yakifanya kazi kwenye barabara ya mradi wa Daraja la 4 la Abidjan huko Abidjan, Cote d'Ivoire. (Zhang Chaoqun/China State Construction Engineering Corporation/ Xinhua)

ABIDJAN - Mradi wa daraja linalojengwa na China nchini Cote d'Ivoire unatazamiwa kubadilisha usafiri kati ya jumuiya kuu za Abidjan, ukitoa njia mbadala kwa Barabara Kuu ya Kaskazini ambayo mara nyingi huwa na msongamano mkubwa.

Daraja hilo la 4 la Abidjan, ambalo sasa limekamilika kwa zaidi ya asilimia 80, litaunganisha Yopougon, eneo kubwa zaidi la mji mkuu wa kiuchumi wa nchi hiyo, na Plateau kupitia Attecoube na Adjame.

Qiao Weidong, mkuu wa mradi wa Shirika la China State Construction Engineering (CSCEC), Tawi la Cote d'Ivoire ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba daraja hilo litakapoanza kutumika, linatarajiwa kuchukua makumi ya maelfu ya magari kila siku, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katika mji huo wenye pilika nyingi wa Afrika Magharibi.

Tan Dengfeng, anayehusika na masuala ya uhusiano wa soko wa mradi huo katika CSCEC, amesema kuwa usafiri wa barabarani huko Abidjan unaleta changamoto kubwa, huku rasi zikigawanya jiji hilo katika kanda kadhaa ambazo zinahitaji kuunganishwa kwa madaraja.

"Wakati wa saa za watumiaji wengi wa barabara, madaraja matatu yaliyopo yanakabiliwa na msongamano mkubwa," Tan amesema.

Luc Koula, mkazi wa eneo hilo, amesisitiza umuhimu wa daraja hilo, akisema kuwa Plateau ni kitovu cha biashara cha jiji hilo na kitovu cha utawala cha serikali. Wakazi wengi wanapaswa kutumia saa mbili hadi tatu kusafiri kutoka Yopougon hadi Plateau kwa kazi, na Barabara kuu ya Kaskazini ikiwa njia kuu. Ingawa vivuko vinapatikana kwa kuvuka rasi, usafiri wa gari ni mzuri zaidi kwa wale wanaoishi maeneo ya ndani zaidi.

Mradi wa Daraja la 4 la Abidjan, lenye urefu wa takriban kilomita 7, ulianza Agosti 2018 ikiwa ni sehemu muhimu ya Mradi wa Usafiri wa Mjini Abidjan.

Mradi huo umetoa fursa za ajira kwa wenyeji 1,500 mjini Abidjan na kusaidia kuzalisha ajira 2,000 za ziada katika sekta zinazohusiana, Qiao amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha