Kongamano la Biashara kati ya Zimbabwe na China lafunguliwa mjini Beijing

(CRI Online) Mei 31, 2023
Kongamano la Biashara kati ya Zimbabwe na China lafunguliwa mjini Beijing

Kongamano la Biashara kati ya Zimbawe na China (Zimbabwe-China Bussiness Forum) limefunguliwa leo Mei 30 kwenye hoteli ya Marriott hapa Beijing.

Akifungua kongamano hilo Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe Dkt. Fredric Shava ambaye yuko ziarani nchini China, amesema China ni mshirika mwenzi muhimu wa biashara, na pia ni chanzo kikuu cha uwekezaji na uhamishwaji wa teknolojia kwa Zimbabwe.

Amesema, katika miaka minne iliyopita, China imewekeza dola za kimarekani bilioni 2.7 nchini Zimbabwe, na Zimbabwe imetoa vibali zaidi ya 400 vya uwekezaji kwa kampuni za China.

Ameongeza kuwa uwekezaji kutoka China umetoa nafasi za ajira, kuhimiza maendeleo ya miundombinu, kuendeleza sekta za madini, viwanda na kilimo na kuzifanya kuwa za kisasa, na hivyo kutoa mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa Zimbabwe.

Dkt. Shava amesisitiza kuwa Zimbabwe itaendelea kuimarisha ushirikiano na China, na kupanua zaidi uwekezaji na biashara kati ya pande hizo mbili.

Wakati wa kongamano hilo litakalofanyika kwa siku tatu hadi Juni 1, wajumbe kutoka wizara, mashirika na makampuni mbalimbali, zikiwemo Wizara za Biashara, Utalii, Kilimo na Madini za Zimbabwe, Benki Kuu ya Zimbabwe, Shirika la Kuhimiza Biashara la Zimbabwe (ZimTrade), Wizara ya Utamaduni na Utalii ya China, Baraza la China la Kukuza Biashara ya Kimataifa na Benki ya EXIM ya China, watabadilishana maoni kwa kina kuhusu namna ya kuhimiza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye nyanja za uwekezaji na biashara, maendeleo ya sekta za kilimo, madini na utalii nchini Zimbabwe.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha