Rais Xi atembelea shule ya Beijing kuelekea siku ya kimataifa ya watoto inayoadhimishwa leo Juni 1

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 01, 2023
Rais Xi atembelea shule ya Beijing kuelekea siku ya kimataifa ya watoto inayoadhimishwa leo Juni 1
Rais Xi Jinping wa China, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC), akizungumza na wanafunzi katika shamba la wanafunzi la Shule ya Yuying ya Beijing Mei 31, 2023. Rais Xi siku ya Jumatano alitembelea Shule ya Yuying ya Beijing na kutoa salamu kwa watoto kote nchini kuelekea Siku ya Watoto ya Kimataifa, ambayo inaadhimishwa leo Juni 1 duniani kote. (Xinhua/Ju Peng)

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping siku ya Jumatano alitembelea Shule ya Yuying ya Beijing na kutoa salamu kwa watoto kote nchini China kuelekea Siku ya Watoto ya Kimataifa, ambayo inaadhimishwa leo Juni 1 duniani kote.

Rais Xi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC) amesisitiza maendeleo ya pande zote ya watoto katika zama mpya, na kutoa salamu za Siku ya Watoto ya Kimataifa kwa watoto kote nchini China.

Katika ziara yake hiyo kwenye Shule ya Yuying ya Beijing, Rais Xi amesema watoto ni mustakabali wa nchi na tumaini la taifa. Amesisitiza umuhimu wa msingi mzuri wa maadili, uwezo wa kiakili, nguvu ya mwili, usikivu wa uzuri na ustadi wa kazi wa watoto.

Amewataka watoto wa China katika zama mpya kuwa na matarajio na matumaini makubwa juu ya siku za baadaye , kufurahia kusoma na kufanya kazi, kuwa na shukrani na rafiki, na kuwa na ujasiri wa kuvumbua na kufanya juhudi kubwa.

Ameeleza matumaini yake kuwa wanafunzi hao watasoma kwa lengo la kujenga nchi yenye nguvu na kuchangia katika ustawishaji wa Taifa la China, na kukidhi matarajio ya wazazi wao, Chama na wananchi.

Shule hiyo ilianzishwa Mwaka 1948 huko Xibaipo, eneo ambalo lilikuwa msingi wa mapinduzi katika Mkoa wa Hebei, Kaskazini mwa China.

Akiwa kwenye makumbusho ya shule hiyo, Rais Xi alifahamishwa kuhusu historia ya shule hiyo, na namna ilivyohimiza mageuzi na uvumbuzi katika elimu na mbinu za kufundishia, na jinsi ilivyotekeleza hatua za kupunguza mzigo wa kazi nyingi za masomo nyumbani na mafunzo ya nje ya muda wa masomo kwa wanafunzi, au "sera ya mapunguzo mawili", katika miaka ya hivi karibuni.

Rais Xi pia amesisitiza juu ya elimu ya michezo ya riadha kwa watoto. Amesema, ni muhimu kuzijaza shule na walimu wa kutosha na wenye uwezo wa michezo ya riadha , na familia, shule na jamii zinapaswa kuweka mazingira bora kwa ajili ya vijana na watoto ili kuboresha utimamu wao wa kimwili.

Wakati akitembelea shamba la wanafunzi shuleni hapo, ambapo wanafunzi wa shule hiyo walikuwa wakijishughulisha na kilimo, Rais Xi amehimiza juhudi za kuwaelekeza watoto ili kukuza ufahamu wa kazi za mikono na kujenga tabia ya kufanya kazi tangu walipokuwa wadogo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha