Peng Liyuan, Mke wa Rais Xi na wake wa marais wa Afrika waanzisha kampeni ya afya kwa watoto yatima barani Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 02, 2023
Peng Liyuan, Mke wa Rais Xi na wake wa marais wa Afrika waanzisha kampeni ya afya kwa watoto yatima barani Afrika
Daktari wa timu ya 22 ya madaktari wa China nchini Cameroon akifanya uchunguzi wa macho kwa mtoto huko Yaounde, Cameroon tarehe 26, Mei. (Picha/Xinhua)

BEIJING - Peng Liyuan, Mke wa Rais wa China Xi Jinping, na Shirika la Wake wa Marais wa Afrika kwa Maendeleo (OAFLAD) kwa pamoja wameanzisha kampeni ya huduma ya afya kwa watoto yatima wa Afrika "Moyo wa Upendo wa Watoto: Hatua za Pamoja kati ya China na Afrika” kabla ya Juni Mosi, Siku ya Watoto ya Kimataifa.

Mabalozi na timu za madaktari wa China katika nchi za Afrika wametembelea watoto katika vituo vya watoto yatima na mashirika yanayohusika, kufanya shughuli kama vile uchunguzi wa afya bila malipo na msaada wa mifuko ya huduma.

Kuhusu shughuli hiyo ya hisani, Peng amesema, China ni rafiki wa kudumu na mshirika wa dhati wa Afrika. Kwamba, mwaka huu inatimia miaka 60 tangu kutumwa kwa timu za madaktari wa China barani Afrika na serikali ya China. Amesema, timu za madaktari wa China zimesaidia kikamilifu watu wa nchi za Afrika na kuwa wajumbe wa kuendeleza urafiki kati ya China na Afrika.

Peng ameeleza matumaini yake kuwa kampeni ya huduma za afya kwa watoto yatima wa Afrika inaweza kupitisha moyo wa upendo na matunzo kwa watoto, kuboresha afya na ustawi wa watoto wa Afrika, na kuchangia katika kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya.

Monica Geingos, mwenyekiti wa zamu wa OAFLAD na mke wa rais wa Namibia, na wanachama wa shirikisho hilo wameitikia vyema na wameelezea shukrani kubwa kwa Peng juu ya huduma na uungaji mkono wake wa muda mrefu kwa maendeleo ya mustakabali wa wanawake na watoto katika Afrika.

Marais, wake wa marais, na maafisa wakuu kutoka nchi nyingi za Afrika wameshiriki kwenye shughuli muhimu zilizofanyika katika nchi zao, ambapo hali ilikuwa ya upendo na yenye mguso. Wamesema urafiki wa kweli haujui umbali na China ni jirani wa karibu ingawa iko umbali wa maelfu ya maili.

Pia wametoa shukrani za dhati kwa China kwa msaada wake wa kujitolea na msaada wake wenye thamani kwa Afrika kwa muda mrefu na wanatarajia kuandika ukurasa mpya wa urafiki kati ya Afrika na China na kujenga mustakabali mzuri pamoja. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha