Mwanadiplomasia wa Trinidad na Tobago achaguliwa kuwa Rais mpya wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 02, 2023
Mwanadiplomasia wa Trinidad na Tobago achaguliwa kuwa Rais mpya wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Dennis Francis, Rais mteule wa Kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akihutubia kikao cha Baraza Kuu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Juni 1, 2023. Mjumbe wa kudumu wa Trinidad na Tobago katika Umoja wa Mataifa, Dennis Francis, amechaguliwa kuwa Rais wa kikao kijacho cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi. (Loey Felipe/Picha ya UN/Kutumwa Xinhua)

UMOJA WA MATAIFA - Mjumbe wa kudumu wa Trinidad na Tobago katika Umoja wa Mataifa, Dennis Francis, amechaguliwa kuwa Rais wa kikao kijacho cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi.

Francis amechaguliwa kwa shangwe katika kikao cha Baraza Kuu, kwa kuwa ugombeaji wake haukupingwa.

Atachukua wadhifa huo mpya Septemba 2023, kumrithi Rais wa sasa wa Baraza Kuu Csaba Korosi, mwanadiplomasia wa Hungary.

"Ninajitolea kutekeleza majukumu ya ofisi kwa uwazi, uwajibikaji, nguvu, na kujitolea, nikikumbuka kwamba nchi wanachama zote zina haki sawa," Francis ameliambia Baraza Kuu baada ya kuchaguliwa kwake.

Francis amesema atatoa kipaumbele katika kuhimiza na kuwezesha mazungumzo yenye maana katika miundo mbalimbali ili kuhakikisha kuwa kuna uwazi wa vipaumbele na uimarishaji wa madhumuni ya pamoja kwa maslahi ya mshikamano.

"Ni matumaini yangu kwa usaidizi na uungaji mkono wenu, kuleta hali mpya ya upatanishi, ushirikiano na kujitolea kwa pamoja katika kutatua changamoto nyingi na kutumia kila fursa, katika kipindi hiki, kabla ya Baraza Kuu." amesema.

Francis ameomba kuungwa mkono na kushirikisha nchi wanachama katika juhudi za kuharakisha hatua za kufikia maendeleo endelevu.

Korosi amempongeza Francis kwa kuchaguliwa kwake.

Francis, balozi aliyefanya kazi kwa muda mrefu zaidi wa Trinidad na Tobago kufikia Mwaka 2016, amekuwa na uzoefu wa kibalozi wa miaka 40 katika huduma ya kidiplomasia nchini humo.

Alikua mwakilishi wa kudumu wa Trinidad na Tobago katika Umoja wa Mataifa mnamo Septemba 2021.

Kati ya Mwaka 2006 na 2011, Francis alikuwa balozi na mwakilishi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa huko Geneva, Shirika la Afya Duniani na Baraza la Haki za Kibinadamu.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha