Mtu mmoja afariki na wengine 5 kujeruhiwa na bango la matangazo lililoporomoka baada ya dhoruba kubwa ya mchanga kupiga Cairo, Misri

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 02, 2023
Mtu mmoja afariki na wengine 5 kujeruhiwa na bango la matangazo lililoporomoka baada ya dhoruba kubwa ya mchanga kupiga Cairo, Misri
Picha iliyopigwa Juni 1, 2023 ikionyesha mabango ya biashara yaliyoporomoka kutokana na dhoruba ya mchanga huko Cairo, Misri. Mtu mmoja ameuawa na wengine watano kujeruhiwa katika Mji Mkuu wa Misri, Cairo baada ya dhoruba kubwa ya mchanga kupiga maeneo kadhaa ya Misri siku ya Alhamisi. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

CAIRO - Mtu mmoja ameuawa na wengine watano kujeruhiwa katika Mji Mkuu wa Misri, Cairo wakati ambapo dhoruba kubwa ya mchanga imepiga maeneo kadhaa ya Misri siku ya Alhamisi na kuendelea leo Ijumaa.

Madhara hayo ya kifo na majeruhi yametokana na kuporomoka kwa bango la matangazo ya biashara kwenye daraja la Oktoba 6 mjini Cairo, kwa mujibu wa habari zilizoripotiwa za vyombo vya habari vya Misri.

Ajali kadhaa za barabarani pia zimeripotiwa kote nchini humo, huku baadhi ya watu wakijeruhiwa lakini hakuna waliokufa, zimesema habari hizo.

Dhoruba hiyo, ambayo imesababisha kufungwa kwa barabara nyingi, bandari na fukwe nchini kote Misri, imesababishwa na kuzuka kwa hali ya hewa ya joto katika eneo la jangwa la magharibi, amesema Eman Shaker, Mkuu wa Kituo cha Kuhisi kwa Mbali cha Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Misri.

"Dhoruba imesababisha kutoona vizuri katika baadhi ya maeneo. Sehemu zilizoathirika zaidi ni Cairo, Suez, Ismailia na Rasi ya Sinai," amesema Shaker.

Ameeleza kuwa, mkandamizo huo wa joto unaotokea katika eneo la jangwa la magharibi kwa kawaida huambatana na kile kinachoitwa "upepo wa Khamaseen" upepo, joto na mchanga mkavu ambao kwa kawaida huvuma nchini Misri katika majira ya mchipuko.

Dhoruba hiyo ya sasa ya mchanga na wimbi la joto vitaendelea hadi leo Ijumaa, Shaker ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha