Ethiopia yafanya mashindano ya "Daraja la Lugha ya Kichina" kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na shule za sekondari za juu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 05, 2023
Ethiopia yafanya mashindano ya
Washindi wa mashindano ya kuzungumza na kufanya maonyesho kwa Lugha ya Kichina yanayofahamika kwa jina la "Daraja la Lugha ya Kichina" wakipokea tuzo mjini Addis Ababa, Ethiopia, Juni 3, 2023. (Xinhua/Wang Ping)

ADDIS ABABA - Mashindano ya "Daraja la Lugha ya Kichina" ambayo ni Mashindano ya Kupima Uelewa wa Lugha ya Kichina kwa wanafunzi wa shule za sekondari za juu na vyuo vikuu vya Ethiopia yamefanyika hapa Jumamosi.

Mashindano hayo yanaandaliwa na Ubalozi wa China nchini Ethiopia, Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa (AAU) na Taasisi ya Confucius katika Taasisi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ya Serikali ya Ethiopia (TVET). Kwenye mashindano hayo, washiriki walipewa changamoto ya kuwasilisha hotuba na onyesho la talanta.

Jumla ya wanafunzi 16 kutoka vyuo vikuu vitatu vya Ethiopia na wanafunzi sita wa shule za sekondari za juu walishiriki mashindano hayo ya kila mwaka ya kuzungumza na kufanya maonyesho ya jukwaani kwa Lugha ya Kichina duniani kote.

Gemechis Melaku, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa lugha ya Kichina katika AAU, alipokea makofi mengi ya pongezi mara kwa mara kutoka kwa watazamaji kwa hotuba yake na onyesho la muziki wa kijadi wa Kichina, na hatimaye alishinda nafasi ya kwanza katika kipengele cha wanafunzi wa chuo kikuu.

"Nimefurahi sana kushinda mashindano haya. Hii ni fursa nzuri sana ya kukuza ujuzi wetu wa lugha ya Kichina na kuongeza zaidi ujuzi na uelewa wetu wa China na utamaduni wa China," Gemechis amesema.

Balozi wa China nchini Ethiopia Zhao Zhiyuan amesema washindani hao watakuwa "mabalozi" wa kuimarisha uhusiano kati ya watu wa nchi hizo mbili.

"Leo, ninyi wanafunzi wapendwa mmeeleza matarajio yenu bora kwa uhusiano uliokomaa zaidi kati ya nchi zetu mbili kwa kutoa hotuba yenye kaulimbiu ya 'Dunia ni familia moja'," Zhao amesema.

Akihutubia hafla hiyo, Terefe Belay, Mkurugenzi wa Udhamini wa Masomo na Uhusiano wa Kimataifa katika Wizara ya Elimu ya Ethiopia, amesema mawasiliano na uhusiano kati ya Ethiopia na China unazidi kutoa msukumo chanya katika sekta ya elimu ya Ethiopia, huku kukiwa na fursa za ufadhili wa masomo zinazoongezeka kwa wanafunzi wa Ethiopia.

Aidha amewapongeza waandaaji wa mashindano hayo kwa kutoa fursa muhimu kwa wanafunzi wa Ethiopia.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha