Iran yafungua tena ubalozi wake nchini Saudi Arabia baada ya kufungwa kwa miaka 7 (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 07, 2023
Iran yafungua tena ubalozi wake nchini Saudi Arabia baada ya kufungwa kwa miaka 7
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Alireza Bigdeli (katikati) na Naibu Waziri wa Masuala ya Ubalozi wa Saudi Arabia Balozi Ali Al-Yousef (wa pili kulia) wakihudhuria hafla ya kufungua tena ubalozi wa Iran mjini Riyadh, Saudi Arabia, Juni 6, 2023. (Xinhua/Wang Haizhou )

RIYADH - Iran imefungua tena ubalozi wake nchini Saudi Arabia siku ya Jumanne baada ya miaka saba ya kufungwa, ikiwa ni karibu miezi mitatu baada ya nchi hizo mbili kukubaliana kurejesha kawaida uhusiano wa pande mbili chini ya makubaliano yaliyowezeshwa kufikiwa na China.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Alireza Bigdeli, alihutubia hafla ya ufunguzi katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, na kuashiria umuhimu wa tukio hilo kwa uhusiano kati ya Saudi Arabia na Iran.

Bigdeli amesema kuwa, kwa kupandishwa tena bendera ya Iran nchini Saudi Arabia na ya Saudi Arabia nchini Iran, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unaingia katika zama mpya.

Ameongeza kuwa diplomasia ni njia bora ya mawasiliano na mazungumzo kati ya nchi mbili, kwa ajili ya kufikia maelewano, utulivu na amani ya pamoja.

Afisa huyo wa Iran amesisitiza kuwa, Iran daima iko tayari kuimarisha uhusiano na majirani zake kwa kuzingatia misingi ya ujirani mwema.

Bigdeli pia amebainisha kuwa kuhimiza uhusiano wa kiuchumi na uwekezaji wa pamoja kutapelekea nchi hizo kuwa karibu zaidi ili kufikia amani na utulivu katika eneo hilo.

Mwezi Machi mjini Beijing, China, nchi za Saudi Arabia na Iran zilifikia makubaliano ya msingi ya kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia na kufungua tena balozi na jumbe zao.

Kwa mujibu wa taarifa ya pande tatu iliyotolewa kwa pamoja kati ya China, Saudi Arabia na Iran, nchi hizo mbili za mwisho zilikubaliana kusuluhisha tofauti zao kwa njia ya mazungumzo na diplomasia, na kwa kuongozwa na uhusiano wao wa kindugu, kwa kuzingatia kanuni na malengo ya Katiba za Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu na mikataba na kanuni za kimataifa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha