Wavuvi wa Korea Kusini wafanya maandamano kupinga Japan kutiririsha maji machafu ya mionzi baharini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 13, 2023
Wavuvi wa Korea Kusini wafanya maandamano kupinga Japan kutiririsha maji machafu ya mionzi baharini
Watu wakitia saini majina yao kupinga mpango wa Japan wa kutiririsha maji machafu yenye mionzi huko Seoul, Korea Kusini, Juni 12, 2023. Maelfu ya wavuvi wa Korea Kusini walikusanyika Jumatatu karibu na jengo la bunge huko Seoul ili kupinga Japan kwa mpango wake wa kutiririsha maji machafu yenye mionzi kutoka Kinu chake cha Nyuklia kisichotumika cha Fukushima Daiichi kwenye Bahari ya Pasifiki. (Xinhua/Wang Yiliang)

SEOUL - Maelfu ya wavuvi wa Korea Kusini walikusanyika Jumatatu karibu na jengo la bunge huko Seoul ili kupinga Japan kwa mpango wake wa kutiririsha maji machafu yenye mionzi kutoka Kinu chake cha Nyuklia kisichotumika cha Fukushima Daiichi kwenye Bahari ya Pasifiki.

Wavuvi hao walishikilia mabango yaliyosomeka "Tunapinga sana utiririshaji wa maji machafu ya Fukushima baharini," na "SOS!! Bahari ya Pasifiki!"

Kim Kwang-shik, mmoja wa wavuvi waliojiunga na maandamano hayo, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba ingawa hakuwa na taarifa za kitaalamu kuhusu maji hayo yenye mionzi, anafahamu vyema ukweli kwamba kutiririshwa kwake kutaleta madhara.

"Kama maji machafu ya Fukushima ni salama (kama inavyodai Japan), yanaweza kuachwa kuhifadhiwa kwenye nchi kavu ya Japan badala ya kutiririshwa baharini," Kim amesema.

Waandaaji wa maandamano walisema, wavuvi na wanaharakati wa kiraia wapatao 2,000 wameshiriki katika maandamano hayo.

Jumuiya ya wavuvi hao imesema katika taarifa yake kwamba serikali ya Japan inapaswa kuja na suluhu, ikiwa ni pamoja na uhifadhi wa muda mrefu kwenye nchi kavu, badala ya kutiririsha maji hayo ya mionzi ambayo yataangamiza maisha yote katika Bahari ya Pasifiki na wavuvi wote wanaoitegemea.

Jumuiya hiyo imeitaka serikali ya Korea Kusini kuwasilisha malalamiko mara moja kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Sheria ya Bahari dhidi ya Japan, ikisema iwapo maji hayo machafu yatatiririshwa, yatatishia maisha ya wavuvi kutokana na kupungua kwa kasi kwa mahitaji ya bidhaa za baharini. 

Uchunguzi wa kura ya maoni uliofanywa na Rsearch View kwa watu wazima 1,000 wa Korea Kusini mwezi uliopita umeonesha kuwa, asilimia 85.4 ya waliohojiwa walipinga Japan kutiririsha maji hayo machafu, na asilimia 72 walisema watapunguza matumizi ya mazao ya baharini kama maji hayo machafu yatatiririshwa baharini.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha