Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aunga mkono kuundwa kwa shirika la usimamizi wa Teknolojia za Akili Bandia (AI)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 14, 2023
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aunga mkono kuundwa kwa shirika la usimamizi wa Teknolojia za Akili Bandia (AI)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kulia) akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Juni 12, 2023. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumatatu ameeleza kuunga mkono kuanzishwa kwa chombo cha usimamizi wa teknolojia za akili bandia (AI) kilicho kama Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki. (Xinhua/Xie E)

UMOJA WA MATAIFA - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumatatu ameeleza kuunga mkono kuanzishwa kwa chombo cha usimamizi wa teknolojia za akili bandia (AI) kilicho kama Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki.

"Ni nia yangu kuunda chombo cha ushauri wa ngazi ya juu kuhusu teknoloja za akili bandia ili kuandaa kwa makini hatua mbalimbali ambazo tutaweza kuchukua ... ninapendelea wazo kwamba tunaweza kuwa na shirika la teknolojia za akili bandia, ambalo ningesema linachochewa na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki lilivyo leo," katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Guterres amesisitiza haja ya kushughulikia madhara makubwa yanayosababishwa na majukwaa ya kidijitali yaliyojaa habari potofu pamoja na wasiwasi juu ya maendeleo ya teknolojia za akili bandia, akipendekeza kanuni za maadili za kimataifa kama suluhu.

Huku akikiri kwamba tahadhari zilizotolewa na wahusika juu ya AI zimekuwa nyingi hata zinawafanya watu wazibe masikio kwani makelele ni makali, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba hazipaswi kupindisha tahadhari kutoka kwenye uharibifu uliopo unaoletwa na teknolojia za kidijitali. "Hazipaswi kutupotezea mwelekeo kutoka kwenye uharibifu ambao teknolojia za kidijitali tayari zinaufanya kwa Dunia yetu," amesema.

Guterres amesisitiza madhara makubwa duniani yanayosababishwa na kuenea kwa chuki na uongo katika anga ya kidijitali, akibainisha kuwa "kuenea kwa chuki na uongo katika anga ya kidijitali kunasababisha madhara makubwa duniani sasa."

Amesisitiza zaidi kwamba "inachochea migogoro, vifo na uharibifu sasa. Inatishia demokrasia na haki za binadamu sasa."

Akitazama siku za mbele, Guterres amedokeza kuwa Kanuni za utendaji wa kutoa habari kikamilifu kwenye majukwaa ya kidijitali ya Umoja wa Mataifa zinawekwa sasa kwa ajili ya maandalizi ya "Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu Wakati Ujao" unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha