

Lugha Nyingine
UNHCR yasema idadi ya watu walioyakimbia makazi yao duniani imefikia rekodi mpya Mwaka 2022
GENEVA - Idadi ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita, mateso, ghasia na ukiukaji wa haki za binadamu ilifikia rekodi ya milioni 108.4 kufikia mwisho wa Mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 19.1 kutoka mwaka uliopita na ongezeko kubwa zaidi kuwahi kutokea, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema Jumatano.
Katika ripoti yake ya kila mwaka inayoitwa "Mwenendo wa Kimataifa wa Watu Kuyakimbia Makazi yao Mwaka 2022," Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) imesema kuwa hali ya ongezeko la watu kulazimika kuyakimbia makazi yao duniani haionyeshi dalili ya kupungua Mwaka 2023 huku kuzuka kwa migogoro nchini Sudan kukisababisha idadi mpya wa watu wanaokimbia makazi yao, na kusukuma idadi ya jumla ya kimataifa kufikia hadi wastani wa milioni 110 kufikia Mei mwaka huu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya jumla hiyo ya wakimbizi duniani, milioni 35.3 walikuwa wakimbizi, ambao walivuka mipaka ya kimataifa kutafuta usalama.
Idadi ya wakimbizi kutoka Ukraine iliongezeka kutoka 27,300 mwishoni mwa Mwaka 2021 hadi milioni 5.7 mwishoni mwa Mwaka 2022 - ikiwakilisha idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wanaokimbia mapigano popote tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Mwishoni mwa Mwaka 2022, inakadiriwa kuwa watu milioni 4.4 duniani kote hawakuwa na utaifa au walikuwa na utaifa ambao haujaamuliwa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 2 zaidi ya mwishoni mwa Mwaka 2021, ripoti hiyo imeonyesha.
Iwe inapimwa kwa njia za kiuchumi au uwiano wa idadi ya watu, nchi zenye kipato cha chini na cha kati duniani ndizo zinazopokea watu wengi zaidi wanaokimbia makazi yao. Nchi 46 zenye maendeleo duni zinachangia chini ya asilimia 1.3 ya Pato la Dunia (GDP), lakini zilihifadhi zaidi ya asilimia 20 ya wakimbizi wote.
"Watu kote duniani wanaendelea kuonyesha ukarimu wa ajabu kwa wakimbizi wanapotoa ulinzi na usaidizi kwa wale wanaohitaji, lakini msaada zaidi wa kimataifa na uwajibikaji wa usawa unahitajika," Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi Filippo Grandi amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma