Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lahimiza hatua zichukuliwe kushughulikia majanga ya mabadiliko ya tabianchi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 16, 2023
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lahimiza hatua zichukuliwe kushughulikia majanga ya mabadiliko ya tabianchi
Picha hii iliyopigwa Juni 13, 2023 ikionyesha mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu matishio ya amani na usalama wa kimataifa unaoangazia mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. (Manuel Elias/Picha ya UN/Xinhua)

UMOJA WA MATAIFA - Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumanne limesisitiza hatari zinazoongezeka za usalama zinazotokana na majanga ya mabadiliko ya tabianchi katika maeneo hatarishi. Wazungumzaji walihimiza sana hatua madhubuti za kushughulikia uhusiano tata kati ya mabadiliko ya tabianchi na migogoro.

Huku takriban watu bilioni 3.5 wakiishi katika maeneo yenye hatari za majanga ya mabadiliko ya tabianchi, hatari zinazohusiana na amani na usalama zinatarajiwa kuongezeka tu, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Operesheni za Amani Jean-Pierre Lacroix ameliambia baraza hilo, akionya kwamba ni lazima hatua zichukuliwe ili kuepusha hali inayozidi kuwa na madhara mabaya.

Majanga ya mabadiliko ya tabianchi yanasababisha hali mbaya ya mazingira ya usalama, kutoka Afghanistan hadi Mali, na tume za kulinda amani za Umoja wa Mataifa zinachukua hatua za kuhimili, kuanzia kupunguza kiwango chake cha utoaji wa kaboni hadi kushughulikia matokeo mengi yanayohusiana.

"Kwa kuzingatia kuongezeka kwa uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi, amani, na usalama, pamoja na mabadiliko mapana ya mienendo ya migogoro katika maeneo tunayofanyia kazi, lazima tuendelee kuhimili," amesema.

Akitoa muhtasari wa juhudi za sasa, Lacroix amesema kuwa ndani ya miaka kadhaa iliyopita, operesheni nyingi za amani za Umoja wa Mataifa zimekabiliwa na hatari kubwa na changamoto za kisiasa.

Kati ya nchi 16 ambazo ziko hatarini zaidi kwa mabadiliko ya tabianchi, tisa zina ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa, amesema, akisisitiza kwamba operesheni nyingi za amani za Umoja wa Mataifa zimewekwa katika mazingira ambayo yameathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi na yenye viwango vya juu vya ukosefu wa usawa wa kijinsia.

"Tume zetu zinashuhudia udhaifu wa pande mbili unaoletwa na mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usalama," amesema, huku akitoa mifano kadhaa.

Katika mkutano rasmi wa pili wa baraza hilo wa Mwaka 2023, wazungumzaji zaidi ya 70, akiwemo Rais wa zamani wa Colombia na mshindi wa Tuzo ya Nobel Juan Manuel Santos, walibadilishana mawazo kuhusu uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na kuzorota kwa usalama.

Santos Amesema kuwa amani inaweza kudumishwa tu ikiwa misitu, ardhi na mito ambayo jamii hutegemea italindwa na kusimamiwa kwa njia endelevu.

"Tunahitaji hatua kali za kisera," amesema. "Lazima tuongeze juhudi zetu siyo tu katika kupunguza na kuhimili hali bali katika suluhu chanya za asili, ikiwa ni pamoja na kuhifadhi misitu, nyanda za juu, miamba ya matumbawe, na mifumo mingine ya ikolojia yenye uadilifu wa hali ya juu ambayo inawapa binadamu hewa safi na maji safi."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha