Wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania waonyesha umahiri wao katika lugha ya Kichina wakati wa mashindano “Daraja la Lugha ya Kichina”

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 19, 2023
Wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania waonyesha umahiri wao katika lugha ya Kichina wakati wa mashindano “Daraja la Lugha ya Kichina”
Wanafunzi wa Tanzania wakionyesha vipaji vyao kwenye Mashindano ya “Daraja la Lugha ya Kichina” jijini Dar es Salaam, Tanzania, Juni 16, 2023. Wanafunzi 12 kutoka vyuo vitatu vya elimu ya juu nchini Tanzania wameonyesha ujuzi wao katika lugha ya Kichina kwenye Mashindano ya 22 ya Daraja la Lugha ya Kichina, ambayo ni mashindano ya umahiri wa Lugha ya Kichina yaliyofanyika hapa Ijumaa. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)

DAR ES SALAAM - Wanafunzi 12 kutoka vyuo vitatu vya elimu ya juu nchini Tanzania wameonyesha ujuzi wao katika lugha ya Kichina kwenye Mashindano ya 22 ya “Daraja la Lugha ya Kichina”, ambayo ni mashindano ya umahiri wa Lugha ya Kichina yaliyofanyika hapa Ijumaa.

Katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Confucius (CI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dodoma na Darasa la Confucius la Chuo Kikuu cha Zanzibar, washiriki walipimwa na jopo la majaji, hasa maafisa Wachina kutoka kampuni za kibiashara za China zilizowekeza Tanzania, katika ujuzi wao wa lugha ya Kichina, ikiwa ni pamoja na kutoa hotuba kwa Lugha ya Kichina, ujuzi kuhusu China na maonyesho ya vipaji ambayo yalilenga kuelewa utamaduni wa China.

Pendo Malangwa, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ameipongeza Taasisi ya Confucius kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha vijana wa Tanzania wanaweza kujifunza lugha ya Kichina ili kuboresha uwezo wao wa kiushindani katika kujiendeleza kikazi hapo baadaye. "Kujifunza lugha ya Kichina ni mbinu mwafaka katika kuendeleza uhusiano kati ya China na Afrika," amesema.

Naye Mratibu wa Mafunzo ya Baada ya Shahada ya Kwanza katika Chuo cha Masuala ya Binadamu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Herbert Ndomba, amesema mashindano hayo yamewapa wanafunzi maarifa kuhusu utamaduni wa China. "Mashindano haya yanasaidia wanafunzi kuimarisha ujuzi wao wa lugha na mawasiliano, ujuzi huu ni muhimu katika maisha yetu ya kila siku na katika soko la ajira," amesema Ndomba.

Wang Siping, Konsela wa Utamaduni katika Ubalozi wa China nchini Tanzania, amewataka vijana wa Tanzania kujitolea katika urafiki kati ya China na Tanzania, na kuwatia moyo wa kuishi kwa kuendana na wakati.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zhang Xiaozhen, amesema madhumuni ya kuandaa mashindano hayo ni kuboresha umahiri na kiwango cha wanafunzi wa Tanzania wanaojifunza Lugha ya Kichina, kuhimiza kikamilifu mabadilishano ya kitamaduni na lugha kama njia ya mawasiliano na utamaduni kama daraja na kuchangia kwenye lengo kuu la urafiki na ushirikiano kati ya China na Tanzania.

Everius Gozibeth Rwabangi, 23, mwanafunzi wa mwaka wa tatu anayesomea Shahada ya Kwanza ya Sanaa na Elimu (Lugha za Kichina na Kiingereza), aliibuka mshindi wa jumla. "Kujifunza Kichina ni kama ufunguo wa milango kwa fursa kadhaa katika biashara zinazosimamiwa na China nchini Tanzania" amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha