Rais Xi Jinping akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Blinken mjini Beijing

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 20, 2023
Rais Xi Jinping akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Blinken mjini Beijing
Rais wa China Xi Jinping akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken aliyefanya ziara mjini Beijing, China, Juni 19, 2023. (Xinhua/Li Xueren)

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken katika Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing siku ya Jumatatu.Kwenye mazungumzo hayo, Rais Xi amesema Dunia ni kubwa sana kiasi cha kutosha kwa China na Marekani kila moja ipate maendeleo yake na kuziwezesha kupata ustawi kwa pamoja. Wachina, kama ilivyo ya Wamarekani, ni watu wenye heshima, wanaojiamini na wanaojitegemea, watu wote wa pande mbili wana haki ya kutafuta maisha bora. "Maslahi ya pamoja ya nchi hizo mbili yanapaswa kuthaminiwa, na mafanikio yao ni fursa badala ya tishio kwa kila mmoja."

Rais Xi amesema jumuiya ya kimataifa kwa ujumla inafuatilia kwa ukaribu hali ya sasa ya uhusiano kati ya China na Marekani. "Haitaki kuona migogoro au mapambano kati ya China na Marekani au kuchagua upande kati ya nchi hizi mbili, na inatarajia nchi hizi mbili kuishi pamoja kwa amani na kuwa na uhusiano na ushirikiano wa kirafiki."

“Nchi hizi mbili zinapaswa kuwa na msimamo wa kuwajibika kwa historia, kwa watu na kwa Dunia, na kushughulikia ipasavyo uhusiano kati ya China na Marekani” Rais Xi amesema, na kuongeza kuwa kwa njia hii, nchi hizi zinaweza kuchangia amani na maendeleo ya kimataifa, na kusaidia kuifanya Dunia inayobadilika na yenye misukosuko, kuwa iliyo thabiti, yenye uhakika na ya kiujenzi zaidi.

Rais Xi amesisitiza kuwa ushindani wa nchi kubwa hauwakilishi mkondo wa zama za sasa, bado hauwezi kutatua matatizo ya Marekani yenyewe au changamoto zinazoikabili Dunia. Amesema, China inaheshimu maslahi ya Marekani na haitafuti kuchochea au kuchukua nafasi ya Marekani, na katika hali hiyo hiyo, Marekani inahitaji kuheshimu China na haipaswi kuathiri haki na maslahi halali ya China. "Hakuna upande unaopaswa kubadili hali ya upande mwingine ili kuendana na nia yake , na zaidi hauruhusiwi kunyima haki halali ya kujiendeleza ya upande mwingine."

Rais Xi ameeleza kuwa pande hizo mbili zinatakiwa kuendelea kujitolea katika kutekeleza makubaliano ya pamoja ambayo yeye na Rais Biden walifikia huko Bali, na kubadilisha kauli zilizotolewa kwa hamasa kuwa vitendo ili kuleta utulivu na kuboresha uhusiano kati ya China na Marekani.

Kwa upande wake, Blinken amewasilisha salamu za Rais Biden kwa Rais Xi. Amesema Rais Biden anaamini kuwa Marekani na China zina wajibu wa kusimamia kwa uwajibikaji uhusiano wao, na hilo ni kwa maslahi ya Marekani, China na Dunia kwa ujumla.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha