

Lugha Nyingine
Palestina yalaani mauaji ya Israel dhidi ya Wapalestina kwenye Ukingo wa Magharibi
![]() |
Moshi ukionekana wakati wa mapigano kati ya Wapalestina na wanajeshi wa Israel katika Mji wa Jenin ulioko Kando ya Magharibi ya Mto Jordan, Juni 19, 2023. (Picha na Ayman Nobani/Xinhua) |
RAMALLAH - Palestina Jumatatu ilieleza kulaani mauaji ya jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina watano na kuwajeruhi makumi ya wengine wakati wa uvamizi katika mji wa kaskazini mwa Kando ya Magharibi ya Mto Jordan wa Jenin na kambi yake ya wakimbizi.
Msemaji wa Ofisi ya Rais wa Palestina Nabil Abu Rudeineh amesema katika taarifa yake kwamba mauaji yanayoendelea kufanywa na Waisraeli dhidi ya Wapalestina ni "majaribio ya kulipua eneo hilo na kuliburuza kuelekea kwenye uwanja wa machafuko."
Siku ya Jumatatu, Wizara ya Afya ya Palestina ilisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba wanajeshi wa Israel waliwaua Wapalestina watano huko Jenin na kuwajeruhi wengine 66, wakiwemo 14 waliokuwa katika hali mbaya.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limethibitisha katika taarifa yake kwamba wanajeshi wawili wa IDF na maafisa watano wa polisi wa mpakani wa Israel wamejeruhiwa wakati wa mapigano hayo, na wote wamekimbizwa hospitali kupokea matibabu.
Vyanzo vya habari kutoka Palestina na Israel vimesema kuwa jeshi la Israel lilivamia eneo la Jenin kwa usaidizi wa tingatinga, droni na helikopta ili kuwatia mbaroni Wapalestina waliokuwa wakisakwa na vikosi vya usalama vya Israel kwa madai ya kuhusika na mashambulizi dhidi ya Waisraeli.
"Wakati wa shughuli hiyo, majibizano makubwa ya risasi yalitokea kati ya vikosi na watu wenye silaha katika eneo hilo. Idadi kubwa ya vilipuzi vilirushwa kwa vikosi. Vikosi vilijibu kwa moto," Jeshi na Polisi wa Mpakani wa Israeli wamesema katika taarifa ya pamoja.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma