

Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa China atoa wito wa ushirikiano zaidi kati ya China na Ujerumani
BERLIN - Waziri Mkuu wa China aliye ziarani nchini Ujerumani Li Qiang amesema siku ya Jumanne kwamba China na Ujerumani zinapaswa kufanya kazi kwa karibu zaidi, kutoa mchango zaidi kwa ajili ya amani na maendeleo ya Dunia, kubeba jukumu la kuleta utulivu katikati ya mabadiliko, na kuharakisha ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kwa binadamu.
Waziri Mkuu Li ameyasema hayo alipokuwa mwenyekiti mwenza wa mazungumzo ya saba kati ya serikali ya China na Ujerumani na Chansela Olaf Scholz wa Ujerumani.
Viongozi hao wawili walipata wasaa wa kusikia ripoti kuhusu maendeleo ya ushirikiano kati ya China na Ujerumani katika nyanja husika kutoka kwa wakuu wa idara 22 zikiwemo za mambo ya nje, uchumi na biashara, viwanda, fedha, haki, usafiri, elimu, sayansi na teknolojia, afya, ulinzi wa mazingira na maendeleo.
Waziri Mkuu Li amesema kuwa mazungumzo hayo yalikuwa yenye ufanisi na ya kisayansi, na yamepata matunda. Amesema, Chini ya hali ya sasa, pande hizo mbili zinapaswa kutumia fursa ya mageuzi ya kijani na kuhimiza uboreshaji wa ushirikiano.
Amependekeza China na Ujerumani ziwe washirika katika maendeleo ya kijani, kuimarisha mawasiliano na uratibu katika masuala ya kijani na mazingira, kuhimiza maendeleo ya teknolojia ya nishati safi na uboreshaji wa teknolojia ya viwanda, na kuimarisha ushirikiano katika nyanja kama vile magari yanayotumia nishati mpya, mambo ya fedha katika sekta yasiyochafua mazingira na masoko ya upande wa tatu.
Kwa upande wake Scholz amesema utaratibu wa mashauriano kati ya serikali hizo mbili unaonyesha umuhimu maalum wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
“Upande wa Ujerumani uko tayari kudumisha mawasiliano ya karibu na China katika masuala yote kati ya nchi hizo mbili na kushughulikia kwa pamoja changamoto za kimataifa kama vile mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula na matatizo ya madeni,” amesema.
Ameeleza kuwa, Ujerumani haina nia ya kutengana kibiashara na China, na iko tayari kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na wa pande nyingi na China ili kuhimiza maendeleo na ustawi wa Dunia.
Baada ya mazungumzo hayo, Li na Scholz walishuhudia utiaji saini wa nyaraka kadhaa za ushirikiano wa nchi mbili katika nyanja mbalimbali.
Kabla ya mazungumzo hayo, Chansela Scholz alifanya hafla kubwa ya kumkaribisha Waziri Mkuu Li kwenye uwanja mbele ya Ofisi ya Chansela wa Ujerumani. Pia, Li alifanya mkutano na Scholz, ambapo walijadili masuala mengi kama vile ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, kubadilishana wafanyakazi na kuimarisha mawasiliano kati ya watu wa pande hizo mbili, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kadhalika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma