

Lugha Nyingine
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa yasema watu 719 wamekamatwa kwenye ghasia za usiku zinazoendelea (3)
![]() |
Mwanamke akitembea kuipita benki iliyoungua huko Nanterre, upande wa Magharibi wa Paris, Ufaransa, Juni 30, 2023. (Xinhua/Gao Jing) |
PARIS - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa imesema Jumapili kwamba, takriban watu 719 wamekamatwa usiku kucha kuanzia Jumamosi hadi Jumapili nchini humo, ikiwa ni usiku wa tano wa ghasia zilizosababishwa na tukio kuhusu kijana mmoja aliyepigwa risasi na kuuawa na polisi.
Wizara hiyo imesema, katika ghasia hizo maofisa wa polisi na askari 45 wamejeruhiwa, na magari 577 na majengo 74 yameteketezwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin amesema usiku wa Jumamosi ulikuwa "tulivu" kuliko Ijumaa usiku wakati watu 1,311 walipokamatwa na magari 1,350 kuchomwa moto.
Darmanin ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii na kusema, Siku ya Jumamosi usiku, askari 45,000 wa vikosi vya usalama vya Ufaransa walitumwa kote nchini humo kukabiliana na ghasia na uporaji, huku takriban askari 7,000 pekee wakiwa Paris na vitongoji vyake.
Waandamanaji hao pia Jumamosi usiku walishambulia nyumba ya meya wa Hay-les-Roses, mji ulioko Kusini mwa vitongoji vya Paris, na kuwajeruhi mke wa meya na mmoja wa watoto wake.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitarajiwa kufanya mazungumzo saa 1:30 jioni kwa saa za Ufaransa siku ya Jumapili na Waziri Mkuu Elizabeth Borne, Waziri wa Mambo ya Ndani Gerald Darmanin, na Waziri wa Sheria Eric Dupond-Moretti.
Jumanne ya wiki iliyopita, polisi wa Ufaransa alifyatua risasi na kumuua kijana huyo mwenye umri wa miaka 17 baada ya kijana huyo kukataa kutii amri ya kusimamisha gari lake.
Polisi huyo aliyefyatua risasi kutoka kwenye bunduki yake baadaye aliwaambia wachunguzi kwamba alichukua hatua hiyo kwa kuhofia gari hilo kusababisha ajali mbaya.
Kuuawa kwa kijana huyo kwa risasi siku ya Jumanne ya wiki iliyopita kumesababisha maandamano na ghasia kote nchini Ufaransa, ambayo yamesababisha polisi kuwakamata maelfu ya watu katika miji mikubwa ya Ufaransa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma