

Lugha Nyingine
Palestina yasitisha mawasiliano na Israel huku kukiwa na mvutano katika Ukingo wa Magharibi (2)
![]() |
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas (wa pili, kulia) akiongoza mkutano wa dharura wa uongozi wa Palestina katika mji wa Ramallah ulioko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Julai 3, 2023. (Ofisi ya Rais wa Palestina/ Xinhua) |
RAMALLAH - Palestina imeamua siku ya Jumatatu kusitisha mawasiliano, mikutano na uratibu wote wa usalama na serikali ya Israel katika kupinga mashambulizi ya kikatili ya Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yaliyosababisha vifo vya Wapalestina wanane na wengine 80 kuwajeruhiwa.
Uamuzi huo umefanywa kwenye mkutano wa dharura wa uongozi wa Palestina ulioongozwa na Rais Mahmoud Abbas katika mji wa Ramallah ulioko Ukingo wa Magharibi, kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa.
Kwenye mkutano huo, Abbas ametoa wito kwa Wapalestina "kusimama kidete na imara, kuungana na kutetea ardhi na ukamilifu wake," shirika la habari la Palestina WAFA limeripoti.
Uongozi wa Palestina "unarudia wito wake kwa jumuiya ya kimataifa kuwalinda watu wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi, Jerusalem na Ukanda wa Gaza," habari hiyo iliyoripotiwa imeongeza.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo rasmi, uongozi wa Palestina umeamua kwenda mara moja kwa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kutekeleza azimio namba 2334 la Baraza la Usalama na maazimio mengine kuhusu kuwalinda Wapalestina.
Siku ya Jumatatu, Jeshi la Israel, likisaidiwa na magari ya kivita, tingatinga, droni, na helikopta, lilifanya shambulio kubwa la kijeshi dhidi ya mji wa Jenin ulioko Kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi na kambi za wakimbizi huko.
Takriban Wapalestina wanane wameuawa na wengine 80 kujeruhiwa katika uvamizi huo, kwa mujibu wa takwimu za hivi punde zilizotolewa na Wizara ya Afya ya Palestina.
Tangu Januari, watu 24, wengi wao Waisraeli, wameuawa katika mashambulizi mbalimbali yaliyofanywa na Wapalestina, na Wapalestina 180, wakiwemo watoto na wanawake, wameuawa na wanajeshi na walowezi wa Israel, kwa mujibu wa takwimu rasmi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma