

Lugha Nyingine
China yapambana na hali mbaya ya hewa huku mvua kubwa inayozidi kunyesha ikileta athari kubwa (2)
![]() |
Wafanyakazi wakikarabati vifaa vya umeme katika Kijiji cha Caotan kilichoko Kitongoji cha Yantouzhai, Eneo la Guzhang la Wilaya inayojiendesha ya Makabila ya Watujia na Wamiao ya Xiangxi, Mkoa wa Hunan, China, Julai 2, 2023. (Xinhua/Chen Zhenhai) |
CHONGQING - China inafanya juhudi zinazoendelea kukabiliana na hali mbaya ya hewa, huku mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha yakisababisha uharibifu katika maeneo ya kusini na katikati mwa China.
Viongozi wa Serikali ya China wameziagiza serikali za mitaa katika ngazi zote kutoa kipaumbele cha juu katika kuhakikisha usalama wa watu na mali zao, na kupunguza hasara kupitia kazi zao za kuzuia mafuriko na kutoa msaada wa maafa.
Duru ya hivi punde ya mvua kubwa iliyonyesha kuanzia Jumatatu imesababisha vifo vya watu 15 na kuwaacha watu wengine wanne kutojulikana walipo katika Mji wa Chongqing, Kusini-Magharibi mwa China, hadi kufikia saa 1 asubuhi Jumatano, viongozi wa eneo hilo wamesema.
Idara ya kukabiliana na hali ya dharura ya Chongqing imesema, Mvua hiyo kubwa, inayoshuhudiwa hasa katika maeneo ya kando ya Mto Changjiang , imesababisha mafuriko na majanga ya kijiolojia, na kutatiza maisha ya zaidi ya watu 130,000 katika wilaya na maeneo 19 .
Mashamba ya mazao yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 7,500 yameharibiwa, idara hiyo imesema katika taarifa yake.
Idara ya kukabiliana na dharura na makao makuu ya kupambana na ukame ya mji huo imeongeza mwitikio wa usaidizi kwa Ngazi ya III, ikitenga zaidi ya vifaa 29,000 vya msaada wa maafa, ikiwa ni pamoja na mahema, blanketi na vitanda vya kukunjwa, kwa aili ya Wilaya ya Wanzhou, ambayo imeathirika zaidi, ambako mvua yenye rekodi ya kiwango cha juu imeshuhudiwa.
Katika mkoa jirani wa Hunan, maisha ya wakazi zaidi ya 100,000 katika Wilaya inayojiendesha ya makabila ya Watujia na Wamiao ya Xiangxi yalitatizwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua. Zaidi ya wakazi 4,200 wamehamishwa hadi maeneo ya muda.
Hasara za moja kwa moja za kiuchumi katika wilaya hiyo zimefikia takriban yuan milioni 617 (dola milioni 85.73 za Kimarekani), takwimu zimeonyesha.
Katika Mkoa wa Sichuan, sehemu zinazopakana na Chongqing, zaidi ya watu 460,000 wameathiriwa na mvua kubwa mwezi huu, idara ya kudhibiti mafuriko na makao makuu ya kupambana na ukame ya mkoa huo ilisema Jumanne.
Katika mkoa huo, kwa ujumla zaidi ya wakazi 85,000 wamehamishwa hadi mahali salama ikiwa ni sehemu ya hatua za tahadhari.
Serikali ya China imetenga Yuan milioni 320 siku ya Jumatano kutoka kwenye mfuko wake mkuu wa msaada wa majanga ya asili ili kusaidia kazi ya utoaji misaada ya majanga ya mafuriko na ya kijiolojia katika maeneo mbalimbali ikiwemo Chongqing na sehemu nyingine za mkoa wa Sichuan.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma