Askari 410 wa China wa kulinda amani nchini Lebanon watunukiwa nishani za amani za Umoja wa Mataifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 06, 2023
Askari 410 wa China wa kulinda amani nchini Lebanon watunukiwa nishani za amani za Umoja wa Mataifa
Askari wa Kikosi cha 21 cha kulinda amani cha China wakifanya gwaride kwenye kambi ya kikosi hicho katika Kijiji cha Hanniyah Kusini mwa Lebanon, Julai 4, 2023. (Picha na Li Zhulin/Xinhua)

BEIRUT - Jumla ya askari 410 wa kikosi cha 21 cha kulinda amani cha China nchini Lebanon wametunukiwa nishani za amani za Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne kwa kujitolea kwao kudumisha utulivu na amani kusini mwa nchi hiyo.

Gwaride la hafla ya utoaji nishani hizo limefanyika kwenye kambi ya walinda amani wa China katika Kijiji cha Hanniyah, Kusini mwa Lebanon ili kuenzi kikosi hicho cha kulinda amani cha China, ambacho ni sehemu ya Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL).

Katika hotuba yake kwenye hafla hiyo, Kamanda wa UNIFIL, Aroldo Lazaro Saenz, ameelezea shukrani zake kwa "kuendelea kuunga mkono na kujitolea kwa ajabu" kwa serikali ya China kwa ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi wa China nchini Lebanon Qian Minjian, Ofisa wa Kijeshi wa Ubalozi wa China nchini humo, Zheng Yuchong, wawakilishi wa Jeshi la Lebanon, maafisa wa serikali na wafanyakazi wa kijeshi na kiraia wa UNIFIL.

Akiwapongeza sana walinda amani hao wa China, Saenz amesema "nishani hii ni ishara ya shukrani kwa kutambua kazi kubwa mliyofanya kwa weledi na azma" katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.

Amewashukuru walinda amani wa China kwa "kufungua njia kwa ajili ya amani ya kudumu Kusini mwa Lebanon" kupitia kazi yao ngumu na ya kitaalamu kuanzia kuondoa mabomu, kusimamia mstari wa kusimamisha vita, ujenzi, msaada wa matibabu hadi misaada ya kibinadamu.

Kikosi cha 21 cha kulinda amani cha China, ambacho kinajumuisha kikosi cha wahandisi wenye majukumu mbalimbali, kikosi cha wahandisi wa ujenzi na kikosi cha matibabu, kimekuwa kikifanya kazi kwenye Ujumbe wa Umoja wa Mataifa tangu Agosti 2022.

Baada ya kukabidhiwa nishani hiyo, afisa mkuu wa kikosi hicho cha China Yan Xiaoliang amesema heshima hiyo ni aina fulani ya msukumo wa kiroho kwa walinda amani wa China, na kuahidi kwamba wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ari hadi siku ya mwisho ya ujumbe wao.

Zaidi ya askari 7,000 wa kulinda amani wa China wametumwa Lebanon tangu Mwaka 2006.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha