

Lugha Nyingine
Ripoti ya Umoja wa Mataifa yatoa wito wa kuongezwa maradufu juhudi za kimataifa ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu (2)
![]() |
Mwalimu wa Afghanistan akiwa anabeba msaada wa kibinadamu huko Mazar-i-Sharif, Mji Mkuu wa Jimbo la Balkh, Afghanistan, Desemba 15, 2021. (Picha na Kawa Basharat/Xinhua) |
UMOJA WA MATAIFA - Dunia inahatarisha kushindwa kufikia kwa kiasi kikubwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) isipokuwa kama hatua za kuharakisha utekelezaji zitachukuliwa, imesema ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumatatu.
SDGs yenye malengo 17 ilipitishwa kwa kauli moja na viongozi wa Dunia Septemba 2015 ili kutumika kama mwongozo wa juhudi za maendeleo ya kimataifa katika miaka inayoelekea Mwaka 2030. Malengo hayo 17 yanalenga kutokomeza umaskini, kupambana na ukosefu wa usawa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa kutumia takwimu na makadirio mpya, ripoti hiyo yenye kichwa kisemacho "Ripoti ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2023: Toleo Maalum" inatoa tathmini ya kina ya hatua zilizopigwa kwenye SDGs.
"Athari za pamoja za majanga ya tabianchi, mgogoro wa Ukraine, mtazamo mbaya wa uchumi wa kimataifa na athari zinazoendelea za janga la UVIKO-19 zimefichua udhaifu wa kimfumo na kuzuia maendeleo kuelekea kutimiza SDGs," ripoti hiyo imesema.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya takriban malengo 140 yanayoweza kutathminiwa, nusu yake yanaonyesha kupotoka kwa wastani au kupindukia kutoka kwenye mwelekeo unaotarajiwa, na zaidi ya asilimia 30 ya malengo hayo hayajapata maendeleo au, mbaya zaidi, yamerudi nyuma chini ya msingi wa Mwaka 2015.
Ripoti imesema kuwa athari za janga la UVIKO-19 zimesimamisha miongo mitatu ya maendeleo thabiti katika kupunguza umaskini uliokithiri, huku idadi ya watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri ikiongezeka kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi.
"Kama hali ya sasa itaendelea, ifikapo Mwaka 2030, watu milioni 575 watabaki katika umaskini uliokithiri na inakadiriwa kuwa watoto na vijana milioni 84 bado hawatakuwa wakisoma shuleni," imesema ripoti hiyo.
Wakati huo huo, ripoti hiyo imetaja maendeleo katika baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na idadi ya watu duniani wanaopata huduma ya umeme imeongezeka kutoka asilimia 87 Mwaka 2015 hadi asilimia 91 Mwaka 2021, na idadi ya watu wanaotumia mtandao wa intaneti imeongezeka kwa asilimia 65 tangu Mwaka 2015, na kufikia watu bilioni 5.3 Mwaka 2022.
"Ninaziomba nchi zote wanachama kuufanya Mwaka 2023 kuwa wakati wa kuanza haraka kufikia maendeleo ya SDGs, ili kuweka mustakabali wa amani na ustawi zaidi kwa wote," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameandika kwenye utangulizi wa ripoti hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma