Iraq yamfukuza Balozi wa Sweden, na kumrudisha nyumbani kaimu balozi wake nchini Sweden kutokana na tukio la kuchoma Qur'an (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 21, 2023
Iraq yamfukuza Balozi wa Sweden, na kumrudisha nyumbani kaimu balozi wake nchini Sweden kutokana na tukio la kuchoma Qur'an
Picha hii iliyopigwa Julai 20, 2023 ikionyesha ubalozi wa Sweden ulioteketezwa kwa moto huko Baghdad, Iraq. (Xinhua/Khalil Dawood)

BAGHDAD - Serikali ya Iraq siku ya Alhamisi imeamua kumtaka balozi wa Sweden nchini humo kuondoka Iraq na kumrudisha nyumbani kaimu balozi wake kutoka Sweden kupinga tukio la kuchomwa moto kwa kitabu kitakatifu cha dini ya Kiislam, Qur'an na bendera ya Iraq nchini Sweden.

Taarifa iliyotolewa na serikali imesema Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia'al-Sudani alitoa maagizo hayo kwa "kujibu idhini ya mara kwa mara ya serikali ya Sweden ya kuchoma Qur'an, kutusi utakatifu wa dini ya Kiislamu, na kuchoma bendera ya Iraq."

Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya serikali, serikali ya Iraq iliitahadharisha serikali ya Sweden Jumatano usiku kupitia njia za kidiplomasia kwamba Iraq itasitisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Sweden iwapo Qur'an itachomwa moto tena katika ardhi yake kwa idhini ya serikali ya Sweden kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.

Alfajiri ya Alhamisi, mamia ya raia wa Iraq walivamia ubalozi wa Sweden mjini Baghdad na kuchoma moto jengo la ubalozi huo, wakipinga tukio la hivi punde la kuchomwa moto Qur'an na bendera ya Iraq na mtu yuleyule aliyechoma Qur'an wiki tatu zilizopita mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Stockholm.

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imelaani uchomaji huo wa ubalozi ikisema uchunguzi utaanzishwa ili kubaini ni nani aliyechoma moto na kuwajibisha wahusika kwa mujibu wa sheria.

Juni 30, waandamanaji wenye hasira walivamia ubalozi wa Sweden nje kidogo ya eneo lenye ngome kubwa la Green Zone katikati mwa Baghdad, baada ya raia wa Sweden mwenye asili ya Iraq kuchana na kuchoma Qur'an mbele ya msikiti huko Stockholm Juni 28 wakati wa maandamano yaliyoidhinishwa na mamlaka husika za Sweden.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha