Ugiriki yawahamisha maelfu ya watalii katika Kisiwa cha Rhodes huku moto wa nyika ukiendelea kuteketeza misitu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 24, 2023
Ugiriki yawahamisha maelfu ya watalii katika Kisiwa cha Rhodes huku moto wa nyika ukiendelea kuteketeza misitu
Picha hii iliyopigwa Julai 22, 2023 ikionyesha moto mkubwa wa nyika ukiteketeza Kisiwa cha Rhodes nchini Ugiriki. (Picha na Argiris Mantikos/Xinhua)

ATHENS – Mamlaka husika za Ugiriki zimesema takriban wakaazi na watu waliokwenda kwa mapumziko ya likizo wapatao 2,000 wamehamishwa kwa njia ya bahari kutoka kwenye maeneo yaliyokumbwa na moto katika Kisiwa cha Rhodes nchini Ugiriki Jumamosi jioni.

Moto huo mkubwa wa nyika katika Kisiwa cha Rhodes umepamba moto tangu Jumanne alasiri na kuteketeza msitu mnene.

Ingawa wazima moto waliweza kuzima milipuko kadhaa ya moto kwenye kisiwa hicho katika siku chache zilizopita, upepo mkali na joto kali imewasha tena moto huo katika upande wa mashariki na kati mwa kisiwa hicho.

Tahadhari za dharura zilitumwa kwa wakazi ukiwataka kuhama vijiji vinne vilivyo kando mwa bahari.

Katika fukwe za Kiotari na Lardo, vyombo vya baharini vya walinzi wa pwani vikisaidiwa na feri na boti za kibinafsi zimehamisha watu hadi maeneo salama. Maelfu ya watu wamehamishwa kwa njia ya nchi kavu hadi maeneo mengine ya kisiwa hicho.

Zaidi ya wazima moto 200 wakiwa na magari 40 ya kuzima moto walikuwa wakifanya kazi kwenye eneo la tukio, wakisaidiwa na ndege tatu na helikopta tano. Kikosi hicho cha zimamoto kinajumuisha wazima moto 31 kutoka Slovakia, wakiwa na magari matano ya zima moto.

"Chini ya asilimia 10 ya nyumba za watalii kisiwani" zimeathiriwa na amri ya kuhamishwa, msemaji wa idara ya zimamoto ya eneo hilo Yannis Artopios amenukuliwa na Shirika la Habari la Athens akisema.

Moto huo wa nyika katika Kisiwa cha Rhodes ni mmoja wa mamia ya mioto iliyozuka kote Ugiriki wiki hii, ikichochewa na hali kavu ya hewa na mazingira kavu kutokana na wimbi la pili la joto ambalo lilifikia nyuzi joto 45 katikati mwa Ugiriki siku ya Jumapili.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha