Mkutano wa UNFSS+2 wasisitiza changamoto za mfumo wa chakula (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 27, 2023
Mkutano wa UNFSS+2 wasisitiza changamoto za mfumo wa chakula
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) Qu Dongyu (wa kwanza kushoto) akizungumza kwenye hafla ya kufungwa kwa Mkutano wa kuhimiza matokeo wa kila miaka miwili wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula (UNFSS+2) mjini Roma, Italia, Juni 26, 2023. (Giulio Napolitano/FAO/Handout via Xinhua)

ROMA - Mkutano wa siku tatu wa kuhimiza matokeo kila baada ya miaka miwili wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula (UNFSS+2) zimesisitiza changamoto zilizopo mbeleni, amesema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) Jumatano.

Mazungumzo hayo yaliyoratibiwa na Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa na kuandaliwa na Italia kwenye makao makuu ya FAO mjini Rome na kuhitimishwa Jumatano, yamehudhuriwa na washiriki zaidi ya 2,000 kutoka nchi 180 -- wakiwemo wakuu wa nchi na serikali 20 na wawakilishi 125 wa ngazi ya mawaziri.

"Natumai wakati huo wa kutathimini matokeo umetoa dirisha kamili la kuona tunasimama wapi, tumefanya nini hadi sasa, na ni kiasi gani tunachohitaji kufanya ili kusonga mbele," Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema kwenye hafla ya kufunga mkutano huo. "Njia ni ndefu na tunahitaji kuharakisha hatua zetu."

Viongozi wengine walioshiriki katika mkutano huo wa siku tatu ni Alvaro Lario, Mkuu wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), na Cindy McCain, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP). FAO, IFAD na WFP ni mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa ya chakula yenye makao yake makuu katika mji mkuu wa Italia, Rome.

Miongoni mwa matokeo muhimu ya mazungumzo hayo ni kubainisha "njia za kitaifa" kukabiliana na vichocheo muhimu vya hali ya ukosefu wa usalama wa chakula na utapiamlo, ambao umechochewa na mabadiliko ya tabianchi, misukosuko ya kiuchumi na migogoro inayoendelea duniani kote.

“Tumesikia changamoto nyingi mnazokabiliana nazo, lakini pia katika kila ugumu fursa huibuka,” amesema Qu.

Mkutano wa UNFSS+2 umeandaliwa kufuatia Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula wa Mwaka 2021, ambao ulianzisha njia ya kubadilisha mifumo ya chakula duniani ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) ya kupunguza umaskini na njaa duniani ifikapo Mwaka 2030.

Hata hivyo, kufikia malengo haya kumekuwa changamoto zaidi tangu kuanza kwa vita kati ya Russia na Ukraine, na kupanda kwa bei ya nishati duniani kote na kushuka kwa ukuaji wa uchumi duniani kote kulikofuata.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha