Lugha Nyingine
Siku ya tatu ya Michezo ya Chengdu Universiade: China inaendelea kuongoza, walenga shabaha wa India wavunja rekodi ya dunia
Timu ya China imeendelea kufanya vizuri katika siku ya 3 ya Michezo ya 31 ya Vyuo vikuu ya Dunia (FISU) inayoendelea mjini Chengdu, na kutwaa mataji manne kati ya 23 yaliyogombewa jumatatu na kuendelea kuongoza kwenye jedwali la orodha ya medali kwa kuwa na 17 za dhahabu.
Korea Kusini iliongeza medali tano za dhahabu (mbili kutoka za mchezo wa taekwondo, mbili za mchezo wa kurusha mishale, na moja ya mchezo wa judo), na sasa imeipiku Japan na kushika nafasi ya pili kwa kuwa na jumla ya dhahabu 13.
Japan ilipata medali mbili zaidi za dhahabu (moja kutoka mchezo wa judo na nyingine jimnastiki), iko katika nafasi ya tatu ikiwa na jumla ya medali 11 za dhahabu.
Walenga shabaha wa India wamevunja rekodi ya dunia ya timu ya wanaume ya kulenga shabaha mita 10 na kupata medali ya dhahabu. India ilijikusanyia pointi 1894.7 na kushinda taji hilo, kwa pointi 7.3 zaidi ya rekodi ya awali ya dunia iliyowekwa na China mwaka 2018. Hata hivyo, kwa kuwa matokeo ya mchezo wa kulenga shabaha ya michezo ya Vyuo Vikuu ya Dunia FISU hayakujumuishwa katika matokeo ya bodi inayoongoza mchezo wa kulenga shabaha kwenye michezo ya Olimpiki (ISSF), matokeo hayo hayahesabiwi kama rekodi mpya ya dunia.
Mlenga shabaha wa India Aishwary Tomar alisema baada ya matokeo hayo, "Nina furaha sana na ninajivunia kupata medali ya dhahabu katika Michezo ya Vyuo Vikuu ya Dunia. Juhudi zangu zimezaa matunda."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma