Makampuni ya China yanatumia maonyesho ya kilimo na biashara ya Zambia kuvutia watu wanaotafuta kazi (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 07, 2023
Makampuni ya China yanatumia maonyesho ya kilimo na biashara ya Zambia kuvutia watu wanaotafuta kazi
Mtu anayetafuta kazi (kushoto) akiongea na mwajiri kwenye maonyesho ya 95 ya Kilimo na Biashara huko Lusaka, Zambia, Agosti 4, 2023. (Picha imepigwa na Martin Mbangweta/Xinhua)

LUSAKA, Agosti 5 (Xinhua) -- Makampuni ya China nchini Zambia, Ijumaa iliyopita yalifanya maonyesho kwenye Maonyesho ya 95 ya Kilimo na Biashara yenye lengo la kuwavutia watu wanaotafuta nafasi za ajira.

Jumla ya makampuni 16 ya China yalishiriki kwenye maonyesho hayo, yaliyoandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara wa China nchini Zambia (CCCZ). Katika siku ya kwanza, mamia ya watu waliokuwa wanatafuta kazi walifurika kwenye banda la China, ambako kampuni hizo zilikuwa zikifanya maonyesho wakitafuta nafasi za ajira.

Mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara wa China nchini Zambia Bw. Li Tie, alisema maonesho hayo yanawakilisha mpango wa kihistoria unaolenga kuziba pengo kati ya waajiri na wanaotafuta nafasi za kazi nchini Zambia.

Amesema jukwaa hilo linatoa fursa za kipekee kwa kampuni za ndani na za kimataifa kutafuta vipaji kwa njia ya kipekee, na wakati huo huo kuhamasisha mageuzi ya kiuchumi kwa kuongeza tija kwa wafanyakazi wenye vipaji watakaobahatika kuajiriwa.

Alisema ukosefu wa ajira unaendelea kuwa tatizo kubwa kwa nchi nyingi duniani, ikiwemo Zambia, na kuongeza kuwa shirika hilo limejitahidi kupigania upatikanaji wa ajira na ukuaji wa uchumi wa Zambia. Pia amesema maonyesho hayo yalilenga kusherehekea moyo wa ushirikiano kati ya China na Zambia, na kuongeza kuwa jukwaa hilo pia limelenga kuwapa watu fursa kuonyesha vipaji na ujuzi wao ili kubadilisha nchi kuwa sehemu yenye uvumbuzi na ujasiriamali.

Waziri wa kazi na hifadhi ya jamii wa Zambia Bibi Brenda Tambatamba, ameyapongeza mashirika ya China kwa kutoa fursa kwa watu wanaotafuta kazi kuunganishwa na wenye makampuni.

Maonyesho hayo ni hatua muhimu ya kukabiliana na ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana nchini Zambia, ambao kwa sasa unafikia asilimia 17.4. Waziri huyo amesema maonesho hayo ni daraja kati ya vyuo vikuu na viwanda, na yanaendana na azma ya serikali ya kuimarisha maendeleo ya watu na ya kijamii, kwa kuwapa vijana ujuzi wa kuwawezesha kushiriki katika shughuli za uchumi.

Wakati huo huo watu wanaotazamiwa kutafuta nafasi za kazi, walionyesha furaha kutokana na fursa zinazotolewa na makampuni ya China. Albert Kazembe aliyekuwa akitafuta kazi ya usimamizi wa maendeleo ya rasilimali watu, alisema alifurahishwa na njia ya uwazi ya kuajiri iliyoonyeshwa na makampuni ya China. Amesema anapenda kufanya kazi kwenye makampuni ya China kwa sababu wachina ni watu wazuri na hawavumilii ufisadi.

Obert Shamulele ambaye alitarajia kupata kazi ya ufundi wa umeme katika moja ya kampuni hizo, alisema anapenda kufanya kazi na wachina kutokana na kujituma kwao katika kazi na kuwa makini. Amesema watu wa Zambia wanahitaji kushirikiana na China ili kuiendeleza Zambia.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha