

Lugha Nyingine
ICRC yapanda mbegu za matumaini kwa wakulima walioathiriwa na mgogoro Cameroon (4)
![]() |
Picha hii iliyopigwa Agosti 7, 2023, inaonyesha eneo la Kerawa la kaskazini mwa Cameroon. (Picha imepigwa na Kepseu/Xinhua) |
Yaoundé, Agosti 13 (Xinhua)
Mkulima mdogo wa eneo lenye mgogoro kaskazini mwa Cameroon Boukara Abba, alikuwa akitazama kwa furaha mahindi yake na bamia, mazao aliyokuwa amepanga kuvuna mwezi ujao.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 31 ni mmoja wa vijana ambao wamebahatika kuwa na mafanikio katika shughuli za kilimo katika eneo lenye hali ngumu ya usalama. Tangu mwaka 2014, eneo kubwa katika eneo hilo limekuwa linakabiliwa na mapigano kati ya kundi la Boko Haram na vikosi vya serikali.
Watu wengi wa jamii za eneo hilo wamekumbwa na ghasia mpya katika miezi ya hivi karibuni. Mgogoro wa matumizi ya silaha umesababisha kuzorota kwa shughuli za kibinadamu na kufanya sekta ya kilimo katika eneo hilo kukabiliwa na changamoto kubwa, kwani zaidi ya nusu ya watu waliokimbia makazi wanatoka katika maeneo ya wakulima.
Kutokana na mpango wa kilimo wa kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), watu waliopoteza makazi yao nchini Cameroon sasa wanaweza kujipatia riziki kupitia kilimo. Bwana Abba ambaye amewahifadhi watu 20 waliopoteza makazi, amesema kabla ya ICRC kufika kwenye eneo lao hakukuwa na mtu wa kuwapatia mbegu za mazao ya kilimo.
Ofisa wa ICRC anayeshughulikia mambo ya kilimo Bw. Nouratou Bouba Hadja amesema hadi kufikia mwaka huu, mpango wa ICRC umewasaidia watu elfu 26 waliokimbia makazi yao, wale wanaorejea kwenye makazi yao na familia zinazowakaribisha, kwa kuwapatia pembejeo za kilimo na fedha ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Bwana Hadja ambaye ni msimamizi wa shughuli za kilimo katika eneo la Abba, amesema pia kuwa wanawasaidia watu hao kwa kuwapatia mbegu za mahindi, bamia, mtama na choroko, na pia wanazipatia mbolea familia zenye vijana zilizokumbwa na mgogoro, kwa kuwa vijana ndio wanahusika zaidi katika mnyororo wa uzalishaji wa kilimo.
Ofisa wa kilimo na maendeleo vijijini katika eneo la kaskazini mwa Cameroon Bw. Simplice Sadou amesema ushirikiano kwenye sekta ya kilimo kati ya serikali ya Cameroon na ICRC, umefanya sekta ya kilimo kuwa na faida, kuwavutia vijana na kufanya eneo hilo kuwa salama zaidi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma