

Lugha Nyingine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran asema uhusiano na Saudi Arabia "unasonga mbele kwa mwelekeo sahihi" (2)
RIYADH - Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema hapa Alhamisi kwamba uhusiano kati ya nchi yake na Saudi Arabia unasonga mbele kwa mwelekeo sahihi na pande zote mbili zitaendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali.
Amir-Abdollahian ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na Faisal bin Farhan Al Saud, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia baada ya kikao chao katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran, ambaye yuko katika ziara yake ya kwanza rasmi nchini Saudi Arabia tangu nchi hizo mbili zikubali kurejesha uhusiano wa kidiplomasia katika makubaliano yaliyoratibiwa na kufanikishwa na China Mwezi Machi mwaka huu, amesema mkutano wake na mwenzake wa Saudi Arabia umekuwa "wenye mafanikio."
“Iran imejipanga kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hizo mbili katika nyanja za usalama na uchumi, na itaunda kamati ya kiufundi na kiutendaji ili kuendeleza utekelezaji wake,” amesema.
Amir-Abdollahian amethibitisha kuwa rais wa Iran atazuru Saudi Arabia hivi karibuni.
Pia ameonyesha uungaji mkono wake kwa Saudi Arabia kuandaa Maonyesho ya Dunia Mwaka 2030.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al Saud huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Saudi Arabia na Iran, amesema kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia na Iran ndiyo ufunguo wa kudumisha usalama wa kikanda.
Amesema Saudi Arabia itadumisha mawasiliano na uratibu na Iran na kuhimiza maendeleo mapya katika uhusiano wa pande mbili juu ya msingi wa kuheshimiana.
Mwanadiplomasia huyo wa Saudi Arabia pia amekaribisha ziara iliyopangwa ya rais wa Iran nchini Saudi Arabia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma